Msemo wa wahenga unasema: “Kile kisichokuua kinakufanya kuwa na nguvu zaidi.”
Msemo mwingine unasema hivi: “Meli bandarini iko salama, lakini haijajengwa kwa ajili ya kubaki bandarini.”
Hiyo ndiyo imekuwa safari ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) – kuchunguza, kuthubutu na kushinikiza mipaka, ingawa ndani ya mipaka husika. Katika mchakato huo tulijikuta tukiungua vidole mara kwa mara.
Tulipoanzisha The Citizen, desturi ilikuwa magazeti ya Kiingereza kuwa katika kurasa pana (broadsheet), na hapa tulikuwa tunanzisha gazeti jembamba (tabloid).
Mtazamo ulikuwa kwamba tabloid haina ya umakini wa kutosha. Lakini waanzilishi walishikilia msimamo wao, wakaja na kaulimbiu ambayo bado inavutia karibu miaka 20 baadaye: “Maudhui ndiyo yanayohesabika.”
Mtazamo huo wa tabloid haukuiua The Citizen, uliifanya kuwa na nguvu zaidi!
Mwaka 2005, wakati uteuzi wa mgombea urais ndani wa chama tawala unapamba moto, MCL ilijikuta matatizoni baada ya kuchapisha picha ambayo baadaye ilithibitishwa kuwa imebadilishwa, ili kumwonyesha mgombea mmoja kwa namna mbaya.
Bodi ya MCL ilichukulia suala hili kwa uzito mkubwa na baada ya kubaini, bila shaka kwamba, mfumo wa uhariri ulikuwa umedhoofishwa. Ilichukua hatua madhubuti dhidi ya wale walioruhusu maudhui hayo kuingia kwenye gazeti chini ya uangalizi wao.
Kama mhariri mchanga, nilikuwa nikitazama kwa makini, nikishuhudia jinsi miundo ya usimamizi ya NMG ilivyokuwa madhubuti na jinsi kanuni zinasimamiwa kuhakikisha tunalinda na kuishi maadili yetu.
Hili halikutumaliza. Tulijifunza somo letu kwa njia ngumu na lilitufanya kuwa na nguvu zaidi katika uchaguzi uliofuata.
Mwaka huohuo tulikumbwa na janga jingine. Hizi zilikuwa siku za awali za NMG kuwekeza katika MCL, ilikuwa imetuma kundi la waandishi wa habari wakuu wa Kenya kusaidia kuratibu shughuli katika kampuni tanzu, hasa kwa gazeti la The Citizen.
Kundi hili lililazimika kurudi Kenya kwa kukosa nyaraka sahihi, hali iliyosababisha pengo kubwa la kiutendaji kwenye chumba cha habari.
Baadaye, Theophil Makunga, ambaye alikuwa amekwenda Nairobi kusaidia kufufua gazeti la Taifa Leo, alilazimika kurudi kusimamia shughuli zote za uhariri katika MCL.
Tulinusurika. Hili halikutumaliza, lilitufanya kuwa na nguvu zaidi.
Mnamo Septemba 2013, miaka miwili tu baada ya kuthibitishwa kushika nafasi ya Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, gazeti la Mwananchi lilifungiwa kuchapishwa kwa siku 14. Hii ilikuwa ubatizo wa moto kwangu.
Marufuku zaidi yalifuata katika miaka iliyofuata, kila mara yakija na sababu tofauti. Wakati huu ilikuwa The Citizen, ambalo lilifungiwa kwa siku saba Februari 2019.
Na Aprili 2020, katikati ya janga la Covid-19, ambapo usambazaji ulikuwa umesimama na watu waliogopa kununua magazeti wakihofia kuambukizwa virusi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilisitisha leseni ya Mwananchi mtandaoni kwa miezi sita. Hii ilikuwa pigo kubwa, kwani maudhui ya mtandaoni ndiyo njia ya uhakika ya kuwafikia wasomaji.
Hata hivyo, tulijikuta tukikabiliana na masuala ya udhibiti na ufuataji wa sheria baada ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016. Hizi zilikuwa nyakati za majaribu.
Tulinusurika kwenye miundo na mifumo iliyokuwa imewekwa wakati huo. Na muhimu zaidi ni masomo tuliyopata kutoka kwa matukio haya. Tulijifunza kukumbatia mawasiliano magumu na wadau muhimu.
Tumepitia haya yote. Hayakutuua, bali yalitufanya kuwa na nguvu zaidi.
Kwa kuangalia nyuma katika siku za awali, pia tulitambuliwa kuwa tunabeba ajenda za kigeni, na kwamba timu iliyopo hapa haikuwa ikifanya uzalishaji wowote wa maana, bali ilikuwa ikikusanya kile kinachodaiwa kuwa kimetolewa kutoka nje ya nchi.
Kwa kujua ukweli, bodi ilimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wakati huo, Francis Nanai na mimi kama Mhariri Mtendaji Mkuu kuongeza juhudi za ushirikishwaji wa wadau wetu, ambayo ilijumuisha kutoka nje zaidi, kuonekana na kueleza sisi ni nani, kwa nini tupo na nani ni nani katika kampuni.
Hii ikiambatana na ziara za wadau kwenye makao makuu yetu ya Tabata, tuliweza kuonyesha kwamba wanawake na wanaume wa Kitanzania walikuwa wakisimamia shughuli zote. Kama tulikosea, ilikuwa ni kwa sababu ya mapungufu yetu ya kibinadamu na kamwe si kwa makusudi. Hili pia halikutumaliza, lilitufanya kuwa na nguvu zaidi.
Novemba 21, 2017, kampuni yetu na kwa kweli sekta ya vyombo vya habari na wenye nia njema, walishangazwa na habari za kutoweka kwa mwandishi wetu, Azory Gwanda kutoka nyumbani kwake karibu na Kibiti, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Kutokuwepo kwake hadi leo kunabaki kuwa fumbo kubwa kwa familia yake, wenzake wa MCL na zaidi. Kama bodi imekuwa ikisema kila wakati, tunaweza tu kutamani suala hili lifikishwe mwisho kwa familia ili waweze kusonga mbele. Hili lilitutikisa sana!
Tulianza mwaka 2018 kwa pigo kubwa lililotupata, ambapo tulilazimika kusimamisha wahariri wakuu wanne kwa madai ya utovu wa nidhamu, mwishoni mwa Januari.
Hili lilinitikisa sana. Tulilazimika kutumia gharama kubwa kuchunguza suala hilo. Walifutiwa mashtaka, wakasafishwa na wakajiunga tena na timu. Tukio hilo lilikuja na likapita, lakini nilipata uzoefu wa jinsi NMG/MCL inaweza kwenda mbali kuwalinda waandishi wake wanapofuata sera ya uhariri. Hili pia halikutumaliza. Kimsingi lilituhakikishia ngao kwa jina la bodi, pale tunapokuwa upande wa haki.
Agosti 29, 2023, moto uliwaka kwenye ghala letu la uzalishaji, ukaharibu hesabu yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni pamoja na sehemu ya mashine ya uchapishaji.
Hii ilivuruga shughuli zetu pamoja na huduma kwa washirika wetu wa uchapishaji kwa mikataba. Tulipona katika tukio hilo, tulijifunza mambo kadhaa. Ni wakati huu niliuona uchungu wa wafanyakazi kwa kampuni yao.
Ndiyo, hii nayo haikutumaliza, ilitufanya kuwa na nguvu zaidi.
Na kana kwamba hilo halikuwa la kutosha, katika robo ya mwisho ya mwaka 2023, tuliamka na habari kwamba Mahakama Kuu ilituchapa na zuio la akaunti zetu. Ilikuwa miezi miwili ya mapambano na usiku wa kukosa usingizi kuhakikisha meli iko kwenye mstari kwani hatukuweza kulipa mishahara kamili na kusimamia gharama za uendeshaji kwa wakati.
Kama wanavyosema, katika kila wingu kuna mwangaza wa fedha. Tulipita kipindi hicho. Tulijifunza masomo yetu. Halikutumaliza, lilitufanya kuwa na nguvu zaidi.
Tumepitia mengi zaidi katika miaka 20 iliyopita. Muda hautaruhusu kugusia kila kitu. Labda niishie kwa kuangalia changamoto nyingine kubwa ambayo haitakwenda mbali muda wowote – ushindani wa kidigitali!
Kama ilivyo kwa kampuni yoyote ya vyombo vya habari duniani, ushindani huu umeathiri vyombo vya habari zaidi pengine kuliko sekta nyingine yoyote.
Lakini tunakabiliana na changamoto hizo kwa uthabiti. Tulianza kwa kubadilisha maudhui yetu kuwa ya kidijitali mwaka 2016/2017. Tukawa chumba cha habari cha kwanza kilichounganisha maudhui nchini Tanzania.
Miaka mitatu baadaye tulipitia upya mpango wetu na tukaanza safari ya mabadiliko ya kidijitali. Hatujafika pale tunapopataka, lakini tayari tumeanza safari. Ushindani wa kidijitali haujatuua hadi sasa, tunazidi kuwa na nguvu kila siku tunapoendelea kupanua bidhaa na huduma zetu.
Kazi yangu, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu – David Waweru, Ali Mwambola (ambaye aligundua uongozi ndani yangu), Sam Shollei, Tido Mhando na Francis Nanai, imekuwa ni kukimbia sehemu yangu katika mbio za MCL, kabla ya kumkabidhi kijiti kwa mkimbiaji anayefuata – ambaye ni Victor Amani Mushi.
Changamoto na kutokuwa na uhakika havitaisha leo. Vitaendelea kubadilika kulingana na muda.
Maandalizi yetu na azma yetu vitatuwezesha kukutana na fursa huku wengine wakisema tumebahatika tu. Tukumbatie changamoto kama vihatarishi vya kujenga uimara na maandalizi yetu.
Endeleeni kujenga pamoja. Endeleeni kuiwezesha taifa!