Wabunge wataka makali bei ya umeme ipungue

Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kukokotoa upya bei ya umeme baada ya mradi wa kufua nishati hiyo wa Julius Nyerere (JNHPP) kukamilika ili kumpa nafuu Mtanzania.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo Agosti 30, 2024, Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka amesema mradi wa JNHPP umeanza uzalishaji umeme wa kutosha na kuna wa ziada.

Kutokana na hilo amehoji, “je, Serikali haioni haja ya kupitie upya ukokotoaji wa bei za uniti na baadaye kushusha bei ili kuleta nafuu kwa Mtanzania?”

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika majibu ya swali hilo amesema gharama za umeme si za uzalishaji peke yake, bali zinahusisha za usambazaji, usafirishaji na uwekezaji.

“Kwa sasa hata uniti ya umeme ambayo wananchi wanatumia imewekewa ruzuku ya Serikali ili bei iweze kupungua. Ndiyo maana nikasema kwa kadri tunavyofanya tathmini, tutaangalia tutakavyochakata lakini hata sasa wananchi wanapata bei hiyo kwa sababu Serikali imeweka ruzuku,” amesema.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha nne cha mkutano wa 16 wa Bunge, jijini Dodoma leo, Agosti 30, 2024. Picha na Hamis Mniha

Hata hivyo, amesema kwa kuangalia bei za nishati hiyo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania ina bei ya chini.

Kapinga amesema wataendelea kuchakata bei ya umeme na kutoa ruzuku ili wananchi waendelee kupata bei ya umeme ambayo ni himilivu.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Suma Fyandomo amehoji ni lini Serikali itashusha bei ya uniti za umeme.

Katika majibu ya swali hilo, Kapinga amesema bei ya uniti ya umeme inapatikana kulingana na gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.

“Bei ya sasa si halisia, ni bei ambayo ina ruzuku za Serikali ndani yake ambayo kwa sasa wastani wa bei ya uniti moja ya umeme yenye ruzuku ni Sh100 (matumizi ya kawaida chini ya uniti 75 kwa mwezi) na bila ruzuku ni Sh292,” amesema. 

Amesema kwa mwananchi anayetumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi, analipa Sh292 kwa uniti moja ya umeme (kuna ruzuku ndani yake) badala ya Sh320 (bila ruzuku).

Hata hivyo, Kapinga amesema wanaendelea kufanya tathmini ya gharama za utoaji huduma za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mara kwa mara.

Amesema pia wataendelea kurekebisha bei kulingana na gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji zitakavyokuwa.

Related Posts