Dar es Salaam. Misingi ya demokrasia na uwajibikaji inajengwa na uchaguzi huru na haki unaotarajiwa kushuhudiwa Novemba mwaka huu, ukihusisha kuchagua viongozi wa ngazi ya mtaa, vijiji na vitongoji.
Uchaguzi huo unatoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kuchagua viongozi wanaowaongoza katika ngazi ya chini ya utawala, jambo linalochangia katika ujenzi wa Taifa linalosimamia haki, usawa na maendeleo endelevu.
Uthibitisho wa mazingira huru na haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024 unatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka anayesema Serikali imewawezesha wasimamizi wa sheria za uchaguzi huo kuweka mazingira huru.
Kwa mujibu wa Mtaka, mazingira huru na haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa yanaimarisha demokrasia kwa kuruhusu wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima.
Takwimu kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zinaonyesha katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, kulikuwa na ongezeko la ushiriki wa wapigakura kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2014.
Hii inaashiria kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa kushiriki katika kuchagua viongozi wanaowaongoza na kuwakilisha masilahi yao, kadhalika wameridhishwa na mazingira ya uchaguzi.
Akitoa hakikisho la uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa huru na wa haki, Mtaka anasema Serikali imewezesha siyo tu kusimamia kanuni na sheria za uchaguzi, bali kuhakikisha mchakato wote unakuwa huru na wa haki.
“Kazi kubwa ya Serikali ni kusimamia kwa sababu uchaguzi unaendeshwa na sheria za uchaguzi, kanuni na kazi ya Serikali ni kuhakikisha sheria zinafuatwa,” anasema.
Kufuatwa kwa kanuni hizo, anaeleza kunaambatana na kuzingatiwa kwa maelekezo yote yanayohusu uchaguzi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na mamlaka nyingine zinazohusika.
Kwa upande wa Mkoa wa Njombe, anasema kitakachofanyika ni kuhakikisha kila kinachopaswa kufuatwa kwa mujibu wa sheria kinazingatiwa.
“Tutahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na haki,” anaeleza.
Hakikisho la Mtaka linaonyesha dalili ya kuchochewa kwa uwajibikaji wa viongozi kwa kuwawezesha wananchi kuwawajibisha kwa njia ya kura.
Viongozi waliochaguliwa kwa njia ya haki wanafahamu kuwa wanawajibika kwa wapigakura na kushindwa kutekeleza majukumu yao inaweza kusababisha kutoshinda tena katika uchaguzi ujao.
Ripoti ya Transparency International Tanzania inakadiria kuwa uchaguzi huru unaweza kupunguza vitendo vya rushwa katika serikali za mitaa kwa asilimia 30.
Hii ni kwa sababu wananchi wanakuwa na uwezo wa kuwaondoa viongozi ambao hawatimizi wajibu wao ipasavyo.
Hata hivyo, aina hiyo ya uchaguzi pia, inachangia kudumisha amani na utulivu wa kisiasa kwa kuwa unawapa wananchi fursa ya kueleza maoni yao na kuchagua viongozi wao kwa njia ya amani.
Takwimu za Kituo cha Utafiti wa Amani (Centre for Peace Research) zinaonyesha katika maeneo ambayo uchaguzi umeendeshwa kwa haki, kumekuwa na upungufu wa migogoro ya kisiasa kwa asilimia 25.
Hii inaonyesha kuwa wananchi wanapokuwa na imani na mchakato wa uchaguzi, kuna uwezekano mdogo wa kutokea kwa vurugu au migogoro.
Uchaguzi huru na haki unatoa nafasi kwa makundi yote ya jamii kushiriki, ikiwemo wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Demokrasia Tanzania (TADS), uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ulikuwa na ongezeko la asilimia 15 la ushiriki wa wanawake ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2014.
Hii inaonyesha uchaguzi huru unatoa nafasi sawa kwa kila mtu kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia na kuchangia maendeleo ya jamii zao.
Uchaguzi huru na haki unalazimisha serikali za mitaa kufanya kazi kwa uwazi zaidi.
Viongozi wanapochaguliwa kwa njia ya haki, wanakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa utawala wao unazingatia kanuni za uwazi na uwajibikaji.
Ripoti za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha serikali za mitaa ambazo zimekuwa na uwazi katika uchaguzi wake zimepunguza upotevu wa fedha za umma kwa asilimia 20.
Hii ni ishara kwamba uchaguzi huru na haki una mchango mkubwa katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
Uhusiano wa uchaguzi na 4R za Rais Samia
Katika maelezo yake, Mtaka anasema atakachofanya ni kuhakikisha 4R za Rais Samia Suluhu Hassan haziishii kusimamiwa pekee, bali zinaakisi haki kwa wagombea wa vyama vyote.
“Wagombea wa vyama vyote wataiona haki yao kwenye sanduku la kura na mimi mwenyewe ni muumini wa uchaguzi wa haki na muumini wa 4R za Rais Samia,” anasema.
Anasema nia yake ni kuithibitishia dunia kuwa 4R (maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya) zinatekelezwa kwa sababu ni moja ya urithi utakaokumbukwa kwa kila kizazi.
Anaeleza wito wake kwa wanasiasa ni kuzingatia uchaguzi hauondoi utu au hali ya kutoaminiana na kuvunjiana heshima.
“Wagombea wa vyama vyote vya siasa ni vyema wakumbuke tuna maisha baada ya uchaguzi. Uchaguzi utulete pamoja na wananchi watusaidie kupata viongozi bora,” anasema.
Anaeleza wananchi wanafahamu changamoto zilizopo katika mitaa, vijiji na vitongoji, hivyo uchaguzi ndiyo jukwaa pekee linalowapa fursa ya kuzitatua.
Mtaka anasema kuna maeneo ambayo Serikali imepeleka fedha nyingi za miradi lakini wananchi hawaridhishwi na usimamizi, pia yapo maeneo yenye migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Ukute kuna mwenyekiti tu si mwaminifu amechukua fedha ameruhusu wafugaji kuingiza ng’ombe shambani inatokea tofauti ya wakulima na wafugaji,” anasema.
Anasisitiza uchaguzi huo ni jukwaa sahihi la wananchi kuwaondoa viongozi waliowaona wana udhaifu katika utendaji ili wawapate wanaostahili kuwaongoza.
“Wito wangu wananchi watumie fursa hii vizuri, kwanza wajitokeze wote, lakini wafanye maamuzi sahihi watupatie viongozi wazuri watakaowezesha kazi za Serikali kwenda vizuri,” anaeleza.