Wakulima wafurahia mazao ya kimkakati kuingizwa stakabadhi ghalani, TMX

Mbeya. Katika kuhakikisha wakulima mkoani Mbeya wananufaika na kilimo chao, Serikali imesema inakusudia kusimamia uingizaji wa mazao yote ya kimkakati kwenye mfumo wa Stakabadhi Ghalani na Soko la Bidhaa (TMX).

Uamuzi huo ambao umewafurahisha wakulima, umekuja baada ya zao la kakao kuonyesha mafanikio kwa kupanda kwa bei kutoka Sh4, 600 hadi zaidi ya Sh26, 000 kwa kilo Juni 2024.

Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayosifika kwa kilimo, ikiwa na baadhi ya mazao yaliyobainishwa kama ya kimkakati, ambayo ni kakao, mpunga, mbaazi na ufuta.

Akizungumza na Mwananchi, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mbeya, Eliah Richard amesema kwa sasa wameanza na zao la kakao, lakini mkakati ni kuongeza mazao mengine.

Amesema kwa kufanya hivyo, watawasaidia wakulima kunufaika na kilimo chao na kuongeza ushindani katika soko la dunia kwa mazao mengine.

“Serikali inakusudia kusimamia mazao yote ya kimkakati kwa kutumia mifumo ya stakabadhi ghalani na TMX ili kuongeza ushindani kwa kuongeza bei, na hivyo kumwezesha mkulima kunufaika na kilimo chake.

“Kwa sasa tumeanza na zao la kakao, baadaye tutaingia kwenye mpunga katika halmashauri za Kyela, Mbarali, na Mbeya DC. Kisha, mazao ya mbaazi na ufuta yatafuata huku tukitoa elimu kuhusu mfumo huu,” amesema Richard.

Mmoja wa wakulima wa mpunga, Dickson Mhagama amesema iwapo utekelezaji huo utafikiwa, mkulima atakuwa na uhakika wa soko ndani na nje, hasa kutokana na baadhi ya misimu ambapo zao hilo limekuwa likishuka bei.

“Pamoja na kupongeza Serikali kwa hatua hiyo, ninashauri kuwepo kwa ushirikishwaji na elimu kwa wakulima wenyewe, kwani kila chenye faida kina changamoto zake. Kwa mfano, katika minada, wateja huwa wanategeana kwenye bei tofauti na matumizi ya boksi,” amesema Mhagama.

Kwa upande wake, Cecilia Raphael amesema kiu ya wakulima wengi ni uhakika wa soko kwa bei nzuri ili waweze kuendesha maisha yao, na kwamba wapo tayari kuuza mazao kwa mfumo huo kulingana na bei ya kuridhisha.

“Tumesikia bei ya kakao inavyowanufaisha wakulima wa Kyela. Hata sisi wakulima wa mazao mengine tunatamani kuwa na soko la uhakika na tupo tayari kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ili kunufaika na kilimo,” amesema Cecilia.

Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Kyela (Kyecu), Nabii Mwakyenda, amesema kwa sasa mazao ya mpunga na mbaazi yanaweza kuingizwa katika mfumo huo na kwamba hamasa iliyopo kwa wakulima ni kuongeza kasi ya uzalishaji.

“Kwa mazao yanayoweza kuingizwa na kupata soko la uhakika na haraka ni mpunga na mbaazi. Tunachoshauri wakulima ni kuongeza kasi ya uzalishaji,” amesema Mwakyenda.

Related Posts