Mbowe: Polisi watoe ushahidi mipango ya maandamano, kikao cha Zoom

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekanusha kufanyika kwa kikao cha viongozi wa chama hicho kupanga maandamano kupitia mtandao wa Zoom, huku akilitaka Jeshi la Polisi kutoa ushahidi wa kikao hicho.

Mbowe amesema hayo kufuatia taarifa ya Polisi iliyotolewa leo Agosti 30, 2024 na Msemaji wake David Misime kuwa viogozi wa chama hicho wamepanga kuandamana nchi nzima na kuvamia vituo vya polisi.

Kwa mujibu wa Misime, hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kutoweka kwa baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deusdedit Soka, Jacob Godwin Mlay and Frank Mbise.

Katika uamuzi uliotolewa na Mahakama Agosti 28, 2024, shauri la kutaka vujana hao ama wapewe dhamana au wafikishwe mahakamani lilitupwa, huku Jeshi la Polisi likipewa amri ya kufanya upelelezi kujua mahali walipo.

Misime amesema Jeshi la Polisi limepokea  amri hiyo na kuongeza nguvu katika upelelezi ambao lilishaanza tangu awali baada ya kuripotiwa kupotea kwa viongozi hao.

“Baada ya maamuzi hayo ya Mahakama Kuu, Jeshi la Polisi limepata taarifa za uhakika za viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya kikao kwa njia ya kielekroniki (Zoom) na kukubaliana kwa vile hawajaridhika na maamuzi hayo ya Mahakama kwa sababu hayakuakisi malengo yao.

Misime amesema Chadema katika kikao hicho walikubaliana kuanza kuhamasisha wafuasi wao chini chini kufanya maandamano ya kuelekea maeneo tofauti zikiwepo ofisi mbalimbali.

“Wahamasishe na kuunda vikundi vya vijana wapatao 20 wavamie vituo vya polisi vilivyopo Jijini Dar es Salaam kwa wakati mmoja.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote atakayeendelea kuratibu, kuhamasisha na kushiriki katika uhalifu huo wa kupangwa, ambao lengo lake ni kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu…atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Jeshi la Polisi lingependa kusisitiza atakayefika kituo chochote cha polisi kwa nia ovu tumejiandaa na atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria,” amesema Misime katika taarifa hiyo.

Akizungumzia na Mwananchi leo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema taarifa ya uongo ya Jeshi la Polisi ni ya uongo.

“Tuko concerned (tunaguswa) kuhusu usalama na haki za viongozi wetu wanaoendelea kutekwa na kupotezwa, lakini hiyo taarifa kwamba sisi tulifaya kikao cha Zoom ni uongo.

“Ninasikitika kwamba Jeshi la Polisi, taasisi muhimu kama hiyo, linaweza kutoa taarifa ya uongo kama hizo mitandaoni na hebu watupe huo ushahidi, hao waliofanya hiyo Zoom ni kina nani, saa ngapi na wakati gani?” amehoji Mbowe.

Amesema kwa sasa yeye yuko nje ya nchi na hakuna kikao walichopanga kukifanya.

“Hao waliofaya Zoom ni kina nani? Mimi kama mwenyekiti sina taarifa, kina nani wanaamua jambo kama hilo?

“Tuko concern na tunawasiliana mmoja mmoja kuhusu hali ya usalama wa viongozi wetu, lakini kwamba kimefayika kikao kikaweka maazimio kwamba tutavamia vituo vya polisi huo ni ujinga tu kwa Jeshi la Polisi lililokosa weledi na linaweza kutoa taarifa kama hizo za uongo,” amesema.

Mbowe amesema taarifa hiyo ya polisi inalenga kukwepa maswali ya msingi ya walipo Soka na wenzake ambao amesisitiza kuwa jeshi hilo ndilo linawashikilia.

“Watoe ushahidi kama wanao lakini la msingi watueleze, Soka na wenzake wako wapi, maana polisi wanajua, waliwachukua na wamewapeleka wapi, waache kutoa kisingizio cha kitoto kama hicho.”

Alipoulizwa kama watawashtaki polisi kwa kuwazushia taarifa za kikao hicho, Mbowe amesema, “hayo ni mambo mengine, lakini kwa sasa nakwambia hizo ni taarifa za uongo na uzushi na kitu kibaya kwa chombo muhimu kama hicho kukisingizia uongo chama cha siasa muhimu kama Chadema.

“Warudi kwenye hoja ya msingi kwamba, Soka, Mlay na Mbise wako wapi? Hii ya kusema Chadema imefanya Zoom meeting ni ujinga usio na kipimo, hatujawahi kufanya na hatujaweka mpango wowote wa kushambulia kituo cha polisi,” amesisistiza.

Related Posts