KINARA wa mabao wa Ligi Kuu na klabu ya Simba, Valentino Mashaka, amefichua siri ya kuanza na moto Msimbazi, akisema hii imetokana na kocha wa timu hiyo, Davids Fadlu anayemtaka kujiongeza uwanjani kwa kukaba pindi hawamiliki mpira, jambo ambalo amekuwa akilifanyia kazi mara kwa mara.
Mashaka aliyetua Simba akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja msimu uliopita, tayari ana mabao mawili katika mechi mbili ambazo timu hiyo imeshacheza hadi sasa, huku akiendelea kuaminiwa na kocha Fadlu aliyesema huwa anawaambia mchezaji wa kisasa ni lazima ajiongeze kwa kukaba timu isipokuwa na mpira.
Nyota huyo mpya wa Msimbazi, alisema Fadlu mara kwa mara amekuwa akimwambia akitaka kufika mbali na kucheza kwa kiwango kikubwa, anapaswa kujifunza kukaba pindi timu inapokuwa haimiliki mpira, kwa kufanya hivyo hakuna kocha hatatamani kumtumia.
“Kocha anasema mchezaji wa kisasa ananyumbulika kufanya mambo mengi, mara nyingi ananiambia niwe nafanya vyote viwili, timu ikiwa na mpira niwe nashambulia kwa kadri niwezavyo na ikinyang’anywa niwe nasaidia kukaba, kitu ambacho kimenibeba kikosini hadi sasa,” alisema .
Mashaka alisema aina ya soka hilo sio ishu kubwa kwake kwani tangu akiwa anacheza Shule za Msingi alikuwa beki wa kati, kabla ya kubadilisga na kuhamia eneo la ushambuliaji, hali iliyomrahisishia kuendana na kile anachotaka kocha.
“Timu za mtaani na shule, sikumbuki vizuri ila kuna siku alikosekana mshambuliaji, kocha akanipanga nikafunga mabao mengi, kuanzia hapo nikawa nacheza nafasi hiyo hadi leo, lakini ikitokea natakiwa kukaba nakaba vizuri tu,” alisema Mashaka aliyemaliza na mabao matano ya Ligi Kuu msimu uliopita akiwa Geita.