Dar es Salaam. Watendaji wa kata na mitaa nchini wamehimizwa kuibeba ajenda ya kupinga ukatili wa kijinsia katika mipango ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Pia wametakiwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuyasaidia kupata uelewa na kuunga mkono jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii.
Wito huo umetolewa Agosti 29, 2024, jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Maendeleo ya Dawati la Jinsia Wilaya ya Ubungo, Hilda Malosha, katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Usawa wa Kijinsia Tanzania (Sukita) kwa viongozi watendaji wa kata, mitaa, na maafisa ustawi.
Mafunzo hayo yalilenga kujadili na kupanga mikakati ya kupambana na vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake, wasichana, na watoto.
Malosha amewasisitiza viongozi hao kuwa mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia inapaswa kutekelezwa kwa vitendo.
“Kama mipango na mikakati ikiwekwa bila utekelezaji wa kila mmoja kwa nafasi yake, itakuwa vigumu kufikia ndoto ya kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili katika jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa kampeni ya kutokomeza ukatili inatakiwa kuanza katika ngazi ya familia, kwani vitendo vya ukatili, hasa dhidi ya watoto, mara nyingi hufanyika katika ngazi hiyo.
“Kisaikolojia, watoto huwa wanamwamini mtu wanayemjua kwa kufikiri hawezi kumdhuru, na ndio maana mara nyingi matukio haya hufanyika katika ngazi ya familia,” amesema Malosha.
Pia amesema ongezeko la matukio ya ukatili linatokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu masuala ya ukatili, ingawa kuna mwamko wa kutoa ripoti juu ya matukio hayo.
“Vilevile, bado hakuna elimu ya kutosha kuhusu sheria zinazotoa ulinzi na ambazo zinazuia utendaji wa matukio hayo, pia baadhi ya jamii bado haziheshimu masuala ya usawa wa kijinsia,” amesema.
Ametoa wito kwa wanajamii kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.
Kwa upande wake, Ofisa Miradi kutoka Sukita, Jamaica Kyando, amesema wameamua kuanza na viongozi hao kwa kuwa wao ndio wako karibu zaidi na wananchi.
“Tumeona ni muhimu kuwajengea uwezo viongozi hao ili waweze kutekeleza ipasavyo mpango mkakati wa Serikali wa kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto,” amesema Kyando.
Mtendaji wa Kata ya Kibamba, Diana Tibaijuka amesema mafunzo hayo yatawaongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao katika kamati za kupambana na ukatili.
“Pia mafunzo haya yatatusaidia kuwajengea uwezo wanajamii ili kuunga mkono mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,” amesema.
Tibaijuka alitoa wito kwa wanajamii kuendelea kutoa taarifa pindi vitendo vya ukatili wa kijinsia vinapojitokeza ili waliohusika waweze kuchukuliwa hatua.