Mbivu mbichi rufaa ya Magoma,Yanga Sept 9

Hatma ya uhalali wa rufaa ya klabu ya Yanga, sasa itajulikana Septemba 9, mwaka huu wakati Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, itakapotoa uamuzi wa pingamizi dhidi ya rufaa hiyo.

Rufaa hiyo imefunguliwa na Juma Ally Magoma na mwenzake Geoffrey Mwaipopo, wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kuiongezea Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo na wenzake muda wa kufungua shauri la maombi ya marejeo.

Klabu hiyo iliomba kuongezewa muda huo ili kufungua shauri hilo la marejeo ua hukumu ya mahakama hiyo iliyobatilisha Katiba yake ya sasa kufuatia kesi ya msingi iliyofunguliwa na Magoma na mwenzake, wakihoji uhalali wa katiba hiyo.

Magoma na mwenzake Mwaipopo hawakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kuiongezea muda bodi hiyo ya Yanga kufungua shauri hilo la marejeo, hivyo wakakimbilia Mahakama Kuu ambako walikata rufaa hiyo.

Wajibu rufaa katika rufaa hiyo ni Bodi hiyo ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga (mjibu rufaa wa kwanza), Fatma Abeid Karume (mjumbe wa bodi hiyo ma mjibu rufaa wa pili).

Wajibu rufaa wengine ni Abeid Abeid na Jabiri Katundu (mjibu rufaa, wa tatu na wa nne mtawalia, ambao pia waliwahi kuwa wajumbe wa bodi ya klabu hiyo.)

Katika rufaa hiyo wanadai kuwa hawakupewa fursa ya kusikilizwa katika mwenendo wa shauri la maombi ya bodi ya wadhamini wa klabu kuongezewa muda wa kufungua shauri la marejeo ya hukumu yao.

Sababu nyingine wanadai kuwa wadhamini hao wa Yanga kufungua shauri hilo la maombi ya marejeo ya hukumu hiyo, bila kutoa sababu za msingi. Vilevile wanadai kuwa hati ya kiapo kilichounga mkono maombi ya kuongezewa muda kuwa na kasoro za kisheria.

Hata hivyo, Bodi ya Wadhamini wa Yanga imewawekea pingamizi la hoja za kisheria kina Magoma dhidi ya rufaa hiyo, ikibainisha hoja mbili. Kwanza inadai kuwa  uamuzi ambao kina Magoma wameukatia rufaa na ya pili wanadai kuwa rufaa hiyo imeshapithwa na tukio.

Piangamizi hilo limesikilizwa leo Ijumaa Agosti 30, 2024 na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi, ambapo mawakili wa pande zote wamechuana kwa hoja za kisheria, kila upande ukipamba kuishawishi mahakama ikubaliane nao.

Wakili wa Bodi ya Wadhamini wa Yanga, Kalaghe Rashid amejenga hoja kutetea sababu hizo za pingamizi huku akirejea vifungu vya sheria na kesi rejea ( kesi zilizokwishaamuriwa na Mahakama Rufani kuhusu sababu hizo za pingamizi walizoziwasilisha.

Hata hivyo, Wakili wa kina Magoma, Jacob Mashenene kwa upande wake, huku naye akirejea vifungu mbalimbali vya sheria na kesi rejea, amejenga hoja kuishawishi mahakama kuwa sababu za hoja za pingamizi hilo hazina mashiko na kwamba nyingine hazikidhi matakwa ya kisheria kuwa pingamizi.

Mama Karume anawakilishwa na Juma Nassoro na Katundu anawakilishwa na Onesmo Mpinzile ambao wameieleza mahakama kuwa wanaunga mkono pingamizi hilo, lakini Abeid hakuwepo wala wakili wake.

Jaji Maghimbi baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo Jaji Maghimbi akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Septemba 9.

Agosti 4, 2022 Magoma na mwenzake Mwaipopo,  wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo walifungua kesi  wakipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.

Hivyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa Katiba ya mwaka 2011 ni batili na wajumbe wa bodi waliopo  kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.

Kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo kwa madai kuwa walipelekewa wito wa Mahakama lakini hawakuitikia.

Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Pamela Mazengo, Agosti 2, 2023, mahaka hiyo ilibatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.

Mahakama hiyo ilikubalina na madai na maombi ya kina Magoma, ikatamka kuwa Katiba ya sasa ya Yanga, (2011) haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968.

Hivyo ilisema kuwa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.

Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika ( mwenyekiti ), Fatma Abeid Aman Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.

Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batili.

Hata hivyo hukumu hiyo haikuwahi kujulikana hadi Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaya ilipoibuka katika vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani hapo kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.

Uongozi wa klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wake wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza kuwa hakuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo.

Hadi wakati huo ilipoupata uamuzi huo ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.

Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga uamuzi huo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.

Kufuatia uamuzi huo ndipo kina Magoma wakakata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Hata hivyo, Agosti 5, 2024, Mahakama ya Kisutu ilisikiliza shauri la maombi ya marejeo la Wadhamini wa Yanga na katika uamuzi wake ilioutoa Agosti 9, 2024, Mahakama hiyo ilikubaliaa na hoja za Yanga ikatengua huku yaka ya awali iliyokuwa imebatilisha Katiba ya Yanga ya sasa.

Related Posts