KAMBAYA AWACHAMBUA WAPINZANI, AWATAKA WATANZANIA WAWAPUUZE

*Aomba msamaha kuwadanganya Watanzania kuhusu Prof .Lipumba na ubobezi wa uchumi…

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

ALIYEKUWA mwanachama wa siku nyingi katika Chama cha Wananchi (CUF) na aliyeshika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama hicho  Abdul  Kambaya ambaye kwa sasa amejiunga na CCM amewataka Watanzania kutopoteza muda wao kwa vyama vya upinzani kwani havina uwezo wa kuongoza wala kuleta maendeleo.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo CPA Amoss Makala, Kambaya ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina udhaifu wa vyama vya upinzani.

“Nimekuwa upinzani na hasa ndani ya CUF nilichobaini hakuna upinzani wa kweli ambao unaweza kupambana na CCM.Vyama vya upinzani na wapinzani wake hawaoneshi kuwa na uongozi wenye wenye tija.”

Amesema katika muda wote wa uwepo wa upinzani wameshindwa kuonesha watafanya nini kwa ajili ya maendeleo lakini hata demokrasia ambayo wanaipigania wameshindwa kuisimamia na wamekuwa wakivurugana kwa kutokuwa na demokrasia ndani ya vyama vyao.

“Viongozi wa vyama vya upinzani hawana demokrasia wamekuwa vyanzo vya migogoro kwa tabia zao za kung’ang’ania madaraka, wengine tangu mfumo wa vyama vingi umeanza wao ndio wamekuwa wenye Viti na akitokea mtu wa kutaka kuwania nafasi hizo wanaanzisha mgogoro.

“Hawaheshimu kabisa demokrasia ndani ya vyama na matokeo yake wenye kuheshimu demokrasia wanaamua kuondoka na kwenda CCM ambako wenyewe demokrasi imepewa nafasi kubwa na ndio maana unaona viongozi wake wanaacha nafasi bila kuwa na malumbano,”amesema Kambaya.

Akifafanua zaidi Kambaya ambaye amekuwa akiamini katika siasa safi na zenye kuangalia maslahi mapana ya Taifa amesisitiza katika matumizi ya demokrasi  kwa maana ya Katiba iliyobora lakini vyama vya upinzani kwa sehemu kubwa Katiba  hazina ukomo wa uongozi na wenye nazo wanapanga watu wao.

“Wameshindwa kufuata Katiba katika maamuzi ya mikutano na kusababisha malumbano lakini wakija kwa Wananchi wanajifanya wanataka Katiba Bora.Katika fedha za umma Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kila anapokagua matumizi ya fedha za vyama hivyo anabaini ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya fedha.

“Wamekuwa wakipata hati chafu kila Mkaguzi anapowakagua . Wameshindwa kuonesha uaminifu wa fedha za umma ambazo wanazipata kama ruzuku. Mwenyekiti wa Chama ndio anajua matumizi ya fedha peke yake na wengine wakihoji inakuwa nongwa,”amesema.

Kambaya ambaye aliwahi  pia kuwa kujiunga na CHADEMA na kwa maelekezo alishindwa kukaa baada ya kuona kuna migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na kufafanua tangu amejiunga CCM amebaini ni Chama ambacho kinaamini katika siasa safi,bora lakini hata viongozi wake Wana maono mapana ya kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo.

Aidha amesema vyama vya Upinzani kikiwemo CUF ambayo yeye alikuwa akikitumikia wameshindwa kuandaa vijana na ndio mana kila anayejitokeza anabanwa na kururudishwa na huo ni mtego ili waendelee kubakia wao.”Kwa msingi huo sioni Watanzania wakipoteza muda kuhangaika  na wapinzani ,watu ambao hata wenyewe hawajui wanataka nini.”

Akizungumzia Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim ambaye katika nafasi hiyo kwa miaka mingi,Kambaya amewaomba msamaha Watanzania kwani akiwa CUF alikuwa akiwaaminisha kuwa Profesa Lipumba ni Msomi mbobezi katika uchumi na amekuwa akishauri mataifa makubwa duniani lakini ukweli ni kwamba alikuwa anawahadaha tu kwani hana uwezo huo.

“Nikiri wakati Niko CUF nilikuwa nafanya kazi ya kuwaaminisha wananchi kuhusu Prof.Lipumba kuwa ni mbobezi katika uchumi,leo naomba niwaambie hana kitu, katika muda wote amekuwa CUF ameshindwa kusaidia Chama kutumia fedha za ruzuku kufanya maendeleo.Ameshindwa kujenga uchumi imara.Kwa kifupi ni msomi aliyeshindwa kusaidia nchi yake

“Ninachoweza kusema na huu ndio ukweli ambao nitausema siku zote upinzani wa nchi hii  umepoteza mtu mmoja muhimu sana ambaye ni Maalim Seif Sharifu Hamad aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF.Alikuwa kiongozi anayejali maslahi ya Taifa.

“Tulikuwa tunapanga mambo lakini Maalim Seif nyakati zote  alitanguliza maslahi ya nchi, alikuwa tayari kupingana na wenzake pale alipoona kuna maamuzi wanataka kufanya lakini yanaviashiria vya kuhatarisha amani au kuharibu utulivu.

” Maalim Seif hakukubali kuona anakuwa sehemu ya kusababisha uvunjifu wa amani lakini alikuwa mkweli.Hawa wengine waliobakia ni viongozi waliopoteza muelekeo na wamebakia kuangalia maslahi yao,”amesema Kambaya.


Related Posts