Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa Marekani Brandon Summerlin(32) kwenda jela miaka 3, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya mescaline zenye uzito wa gramu 56.04.
Pia, Mahakama hiyo imetoa amri ya kuharibu au kuteketeza dawa hizo kwa mujibu wa Sheria za Dawa za Kulevya.
Summerlin alikuwa anakabiliwa shtaka moja la kusafirisha dawa hizo, tukio alilolitenda Novemba 12, 2022 eneo la Posta, Wilaya ya Ilala.
Siku hiyo, mshtakiwa alikutwa akiwa anachukua kifurushi chenye dawa hizo ambazo aliziagiza kutoka Peru.
Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Fahamu Kibona wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali baada ya Mahakama kumtia hatiani, alisema Mahakama hiyo ifanye inavyoona inafaa katika kutoa adhabu yake.
Hakimu Kibona alisema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
Akisoma hukumu, Hakimu Kibona amesema upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi tisa na vielelezo saba.
Alisema kwa upande wa utetezi mshtakiwa ambaye alikuwa anatetewa na Wakili Faith Mwakoti, alijitetea pekee yake na baada ya kumaliza alifunga ushahidi wake.
Alisema katika utetezi wake mshtakiwa aliieleza Mahakama kuwa dawa hizo alikuwa anazitumia kama kiburudisho cha kumsaidia kutulia (ku-relax).
“Mahakama imepitia ushahidi na vielelezo zilivyotolewa na upande wa mashtaka na kujiridhisha na ushahidi huu, hivyo mshtakiwa unatiwa hatiani kama alivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Kibona.
Mahakama baada ya mkutia hatiani, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Judith Kyamba na Aaron Titus uliwasilisha maombi matatu likiwemo la kuiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
“Madhara ya dawa za kulevya kama yalivyo elezwa katika taarifa ya mkemia yanasababisha ulevi usioponyeka, yanasababisha kuharibikiwa na akili na ni dawa ambazo zipo katika kundi la sumu, hivyo athari zake ni mbaya na zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu,” ameeleza wakili huyo.
Pia, Wakili Titus amesema dawa hizo za kulevya zinaharibu akili ya vijana ambao ni nguvu kazi kwa Taifa katika ukuaji wa uchumi katika jamii.
“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka pia tunaomba Mahakama yako tukufu itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wale ambao wanafanya biashara ya dawa za kulevya au kwa wale wenyewe mpango wa kujiingiza kwenye biashara hii haramu,” ameomba.
Hakimu Kibona baada ya kusikiliza maombi ya upande wa mashtaka na ya upande wa utetezi, amesema Mahakama imezingatia maoni ya upande wa mashtaka kuhusu athari za dawa za kulevya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimataifa pamoja na utetezi wa mshtakiwa
“Katika kuzingatia maoni ya pande zote mbili, mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa Summerlin ili iwe fundisho kwa watu wengine na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hujaridhika na adhabu iliyotolewa,” amesema Hakimu Kibona.
“Pia naelekeza dawa za hizo za kulevya aina ya mescaline ziteketezwa kwa mujibu wa sheria za dawa za kulevya,” ameongeza hakimu.
Mshtakiwa alikamatwa na maofisa kutoka Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ( DCEA).