Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko ameomba mwongozo wa Spika akitaka makandarasi wa ndani kulipwa kwa wakati au kulipwa riba pale malipo yao yanapochelewa kama ilivyo kwa wa kigeni.
Matiko akitumia kanuni ya 76 aliomba mwongozo wa Spika kuhusu utata wa majibu ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Bupe Mwakang’ata.
Mwakang’ata aliuliza swali la nyongeza kwenye swali la msingi namba 66 lililoulizwa na mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso kuhusu malipo ya makandarasi wazawa.
Mwakang’ata alitaka kujua ni kwa nini makandarasi wa nje wanapocheleweshewa malipo hulipwa na riba, lakini wa ndani wanapocheleweshwa hawalipwi riba.
“Nimesimama kwa sababu majibu ya waziri kwa kweli si kwamba yanasikitisha lakini yanakatisha tamaa kwa makandarasi wazawa.
“Waziri wa Fedha anasema wanafanya wanayoyafanya kwa sababu makandarasi wa nje wanapoingia mikataba ya kufanya kazi, wanafuata viwango vya kimataifa, lakini makandarasi wa ndani kwa taratibu zilizopo ndizo zinazowataka hata wakicheleweshewa wasilipwe riba,” amesema Matiko.
Amesema wabunge wamekuwa wakipokea malalamiko mengi ya makandarasi wa ndani ya kutolipwa kwa wakati, baadhi inapita miaka mitano na hata saba bila kulipwa.
“Makandarasi wa ndani unakuta wamekopa fedha na wakati mwingine wanatelekeza kazi au wanafanya kazi zao kwa kiwango cha chini. “Nimesimama kuomba mwongozo wako, makandarasi wetu wazawa lazima tuwatie moyo, tumewasomesha na wanavyopata kazi zaidi na kulipwa kwa wakati ndiyo wanavyopata ujuzi zaidi,” amesema.
Amemuomba Spika aielekeze Serikali kutoa usawa kwa makandarasi wote wa ndani na wazawa.
Dk Mwigulu akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa amesema Serikali haipingi hoja ya Matiko.
“Bunge lililopita Serikali tulileta marekebisho ya sheria ili kuwabeba makandarasi wazawa. Na haya yalikuwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunajenga uchumi wetu kwa kuwawezesha wakandarasi wazawa.
“Kwa hiyo, alichosema mbunge na ambacho Bunge linataka ndicho na sisi Serikali tunachosisitiza. Kwa hiyo, rai yangu kwa makandarasi wenyewe Watanzania wajiamini. Kwa mfano, tuna mikataba ambayo ni kati ya mkandarasi na Serikali, na tuna mikataba ambayo ni ya mkandarasi mzawa na mkandarasi wa nje,” amesema.
Dk Mwigulu amesema hutokea makandarasi wazawa huingia mikataba na wa nje na hawaweki ukomo, na Serikali inapowalipa wa nje kwa Dola wao huchelewa kuwalipa wazawa.
“Sasa ambacho tumeelekeza hata wale wa nje, kuepuka kuweka vifungu ambavyo vinaweza vikaepukika kama ambavyo wamefanya wenzetu wa Wizara ya Kilimo kwenye miradi ya umwagiliaji,” amesema.
“Waziri amesema wamechukua hoja ya Matiko, sasa ni kazi yetu kama Bunge kuendelea kufuatilia, sijajua vizuri kwa sababu ile sheria siko nayo hapa, kama ni sheria ndiyo inayosema wale wanaruhusiwa kuweka riba halafu hawa wa ndani hawaruhusiwi kuweka riba au ni utaratibu ambao Serikali imeuweka.
“Lakini, kwa maelezo aliyoyatoa waziri ni kwamba, Serikali inao utayari wa kubadili utaratibu huo ambao umewekwa, sasa sijajua kama umewekwa kisheria. Kwa hiyo, Serikali itazame haya ili hawa wawe wanafanana.
“Kama ni ya kisheria basi Bunge tubadili na Serikali italeta muswada kwa kuwa imeshasema wanao utayari na kama ni utaratibu ambao wameweka ndani ya Serikali waziri amesema wanao utayari wa kubadili na wataenda kubadili,” amesema.