PAMOJA na ukimya uliotawala kwa Mbeya City, lakini benchi la ufundi limesema kimya hicho ni cha kishindo, huku likitambia kambi waliyopo ya Mwakaleli, iliyopo mji mdogo wa Tukuyu mkoani Mbeya, huku Kipa Mnigeria, Olonade Nathaniel akishtua.
Mbeya City iliyoshuka daraja misimu miwili nyuma, imepania kurejea tena Ligi Kuu ambapo inaendelea na mazoezi kwa ajili ya msimu ujao wa Championship kuhakikisha inafikia malengo.
Meneja wa timu hiyo, Mwagane Yeya alisema waliamua kujificha vijijini huko, ili kuweka utulivu kwa wachezaji na kumpa nafasi kocha mkuu, Salum Mayanga kutengeneza kikosi.
Alisema timu hiyo inatarajia kurejea jijini hapa Septemba 3 kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Real Nakonde kutoka Zambia utakaoambatana na utambulisho wa wachezaji na uzinduzi wa jezi.
“Tunaendelea na mipango yetu kimyakimya kwa sababu Championship tunaijua sana, tumeamua kujificha huku kuweka utulivu kwa vijana na kujenga timu, mashabiki watulie mazuri yanakuja,” alisema Yeya.
Nyota huyo wa zamani wa timu hiyo, aliongeza ishu ya usajili viongozi wamejitahidi kuweka wachezaji mchanganyiko wakiwa ni wazoefu na chipukizi kulingana na uhitaji wa ligi.
Alisema katika kuhakikisha City inafanya vizuri wameamua kuvuka mipaka ya nchi kumfuata kipa raia wa Nigeria, Nathaniel ambaye wamejiridhisha ubora wake na ataipa makubwa timu hiyo.
“Sehemu ya usajili uongozi tunawashukuru wametupa tulichohitaji, hatutaki tena sababu, kimsingi hadi sasa hata ligi ikianza sisi tuko tayari na wote wana ari na morali,” alisema Mwagane mmoja ya wachezaji walioipandisha City Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 na kumaliza nafasi ya tatu kabla ya mambo kuwaendea mrama misimu miwili iliyopita iliposhindwa kushikilia bomba na kushuka daraja kupitia play-off dhidi ya Mashujaa iliyochukua nafasi yao.