Dodoma. Bunge limepitisha muswada wa sheria zinazohusu ulinzi wa mtoto, ikiwamo adhabu ya kulipa fidia kwa waathirika, kuanzisha mabaraza ya watoto na mahakama zao kila wilaya.
Muswada huo unaosubiri kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria kamili, pia unatoa mamlaka kwa mahakama kufuta amri ya kuasili mtoto baada ya kupokea maombi ya mzazi, mlezi au ndugu.
Hata hivyo, muswada huo haukuwa na marekebisho kuhusu vifungu vya 13 hadi 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, vinavyobainisha kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi au amri ya mahakama.
Hoja hiyo imekuwa ikipigiwa kelele na wabunge wengi wakitaka marekebisho ya sheria hiyo ambayo inaruhusu mtoto wa kiume kuoa akiwa na umri wa miaka 18.
Muswada huo wa sheria umewasilishwa bungeni leo Agosti 30, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kwa ajili ya kuupitisha katika hatua ya kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu na hatimaye marekebisho yanayopendekezwa yawe sehemu ya sheria za nchi.
Muswada huo umependekeza kufanya marekebisho ya sheria tatu ambazo ni Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura ya 443, Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.
Kifungu kipya cha 71A kinapendekezwa kuongezwa kwa lengo la kuipa mahakama mamlaka ya kufuta amri ya kuasili kwa manufaa ya mtoto baada ya kupokea maombi kutoka kwa mzazi, mlezi au ndugu wa mtoto aliyeasiliwa au mtu mwingine yeyote mwenye masilahi.
Kwa mujibu wa Dk Gwajima, Serikali imerekebisha Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 ambayo sasa mahakama itakuwa na uwezo wa kubatilisha amri ya kuasili mtoto baada ya kupokea maombi kutoka kwa mzazi, mlezi, ndugu wa mtoto aliyeasiliwa au mtu mwingine yeyote mwenye masilahi endapo itaonekana masilahi ya mtoto hayajazingatiwa.
Amesema maombi ya kubatilisha amri ya kuasili mtoto yanaweza kufanywa kabla ya mtoto aliyeasiliwa hajafikisha umri wa miaka 24.
Kwa mujibu wa Dk Gwajima, marekebisho mengine ni kupunguza muda wa mwombaji wa kuasili mtoto asiye Mtanzania kukaa nchini kutoka miaka mitatu hadi miaka miwili.
Muswada pia umefanya marekebisho na kuanzisha mabaraza ya watoto katika kila kijiji, kata, wilaya, mkoa, na katika ngazi ya Taifa ikiwa na lengo la kuanzisha majukwaa yatakayoweza kujua changamoto zinazowakabili watoto na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji unaofanywa katika jamii.
“Lengo la marekebisho haya ni kuwa na majukwaa yanayowafikia watoto na kujua changamoto zinazowakabili ili kuwalinda na matukio ya unyanyasaji na uhalifu katika jamii,” amesema.
Dk Gwajima amesema marekebisho hayo yamepanua wigo wa makosa ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kwa kuongeza makosa mengine sita.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ulinzi wa watoto dhidi ya uhalifu wa kingono ambao umeongezeka kwa kasi kutokana na kukua kwa teknolojia.
“Kifungu cha 97 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuanzisha na kutambua Mahakama za Watoto katika kila wilaya. Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha utoaji haki kwa watoto kwa wakati na kuboresha ustawi na masilahi ya watoto.
“Vilevile, marekebisho haya yanalenga kuzingatia mikataba ya kimataifa kuhusu haki za watoto inayoelekeza nchi wanachama kuwa na Mahakama za Watoto kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya watoto,” amesema.
Amesema kifungu cha 102 kimerekebishwa kwa lengo la kumlinda mtoto dhidi ya uhalifu kwa kutoruhusu kuchangamana na wahalifu ambao ni watu wazima hata kama ni ndugu.
“Kifungu cha 103 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuweka masharti kwa mahakama kuhusu kuahirisha kesi zinazowahusu watoto wanaotuhumiwa kutenda makosa ya mauaji.
“Lengo la marekebisho haya ni kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya watoto na kuwalinda watoto hao dhidi ya kujifunza tabia za uhalifu gerezani,” amesema.
Muswada huo umeweka utaratibu wa mtoto kurekebishwa nje ya mfumo wa mahakama kwa makosa madogo kumsaidia kubadilika kitabia kupitia mifumo ya jamii iliyopo, zikiwamo ofisi za ustawi wa jamii, na vilevile kupunguza muda na gharama za uendeshaji wa kesi za watoto.
Marekebisho mengine ni kwa lengo la kumlinda mtoto ambaye amekinzana na sheria kwa kuhakikisha uwepo wa ofisa ustawi wa jamii katika shauri linalohusisha mtoto.
“Kwa sasa masharti haya yapo kwa mahakama za watoto pekee na si katika mahakama za kawaida,” amesema.
Amesema marekebisho hayo yanampa Jaji Mkuu mamlaka ya kutengeneza kanuni zitakazoainisha utaratibu wa kuwadodosa watoto mahakamani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq akiwasilisha maoni ya kamati amesema suala la fidia kwa mtoto aliyeathirika na vitendo vya kikatili ni maoni yao atakayekutwa na hatia alazimishwe kulipa fidia.
“Kifungu hiki kirekebishwe ili Mahakama imlazimishe mkosaji kumlipa fidia mtoto aliyeathirika na kitendo cha ukatili kwa kutumia neno ‘shall’ na siyo ‘may’ kama ilivyotumika kwenye muswada,” amesema.
Toufiq amesema kamati imetaka maombi ya kubatilisha amri ya kuasili yafanyike kabla mtoto hajafikia miaka 18 na si kabla ya miaka 24.
“Katika Ibara ya 24, kamati ilipendekeza kufuta pendekezo la kupunguza muda unaotakiwa kwa mwombaji asiye Mtanzania kukaa nchini kutoka miaka mitatu hadi miwili mfululilzo na badala yake kuacha miaka mitatu kama ilivyo kwenye sheria.
“Pendekezo hili la kamati linalenga kuhakikisha mamlaka husika zinapata muda wa kutosha wa kujiridhisha na mtu anayetaka kuasili mtoto,” amesema.
Kuhusu uanzishaji wa mabaraza ya watoto, amesema ushauri wa kamati ni kuongeza aya mpya itakayompa waziri mwenye dhamana mamlaka ya kutengeneza kanuni za uendeshaji wa mabaraza hayo.
“Mapendekezo ya kamati yanalenga kuwepo kwa kanuni zitakazofafanua undeshaji wa mabaraza haya,” amesema.
Pia, kamati imeshauri sheria zote zinazohusu masuala ya watoto zipitiwe upya kwa lengo la kuhusianisha na kusomana kulingana na mazingira ya sasa.
“Serikali ione umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya kuendesha mabaraza ya watoto yaliyoanzishwa kwenye sheria hii,” amesema.
Pia, kutokana na majukumu aliyoongezewa Ofisa Ustawi wa Jamii, imependekeza Serikali ione umuhimu wa kuajiri maofisa hao. Kwa sasa kuna upungufu wa asilimia 95.3 ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.