Madiwani Musoma waunda kamati kuhesabu mitumbwi

Musoma. Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini limeunda kamati ya watu wanne kwa ajili ya kufuatilia na kufanya tathmini ya idadi halisi ya mitumbwi katika mialo na visiwa vya halmashauri hiyo, baada aya kutilia shaka idadi iliyowasilishwa na Idara ya Uvuvi.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya madiwani kudai kutokuwa na uhakika na takwimu zilizotolewa na Idara ya Uvuvi, ambazo zilionyesha kuwa kuna mitumbwi 2,300 katika halmashauri hiyo.

Akizungumza leo Ijumaa, Agosti 30, 2024, katika kikao cha kufunga hesabu za mwaka 2023/24, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Charles Magoma amesema kamati hiyo inatakiwa kukamilisha kazi ndani ya wiki mbili.

“Sio kwamba hatuna imani na Idara ya Uvuvi, bali kamati itajumuisha madiwani wawili na wataalamu wawili. Matokeo ya tathmini yao yataletwa kwenye kikao kijacho cha baraza kwa ajili ya taratibu zingine, ikiwa ni pamoja na kuweka mipango mahsusi kwa ajili ya kuimarisha mapato yatokanayo na leseni za mitumbwi,” amesema Magoma.

Halmashauri ya Musoma Vijijini inatoza Sh100, 000 kwa leseni ya uvuvi kwa mtumbwi mmoja kwa mwaka.

Katika bajeti ya mwaka 2023/24, ilikadiria kukusanya Sh240 milioni kutokana na leseni za uvuvi, lakini makadirio hayo yalifikiwa kwa asilimia 70 pekee.

Awali, Idara ya Uvuvi iliwasilisha taarifa kuwa kuna mitumbwi 1,700, lakini baada ya tathmini mpya, idadi iliongezeka hadi 2,300, jambo ambalo lilizua mashaka zaidi.

Magoma alieleza kuwa madiwani wa halmashauri hiyo ni wazoefu katika masuala ya uvuvi, na hivyo walipoona kutofautiana kwa takwimu hizo, waliamua kuunda kamati ifanye tathmini ya kina ili kupata takwimu sahihi, zitakazosaidia kupanga mipango inayoendana na hali halisi.

Diwani wa Ifulifu, Gerald Kasonyi, amesisitiza kuwa idadi ya mitumbwi katika halmashauri yao ni kubwa zaidi ya takwimu zilizotolewa, akiongeza kuwa kati ya kata 21 za halmashauri hiyo, ni kata tatu tu hazina mialo.

Diwani wa Suguti, Jogoro Kulembwa, amesema anaamini kuwa takwimu sahihi zikipatikana, mapato yatokanayo na mitumbwi yatapanda zaidi, na hivyo halmashauri itakuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mingi ya kijamii.

Related Posts