Dora wa Jua Kali yeye na Pacome tu!

MSANII nyota wa filamu nchini anayetamba kwenye tamthilia ya Jua Kali, Wanswekula Zacharia ‘Dora’ humwambii kitu kuhusiana na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua anayemkosha kutokana na aina yake ya uchezaji uwanjani.

Dora akijibu swali aliloulizwa na Mwanaspoti wakati akiwa live katika mtandao wa TikTok juu ya mchezaji gani Tanzania anakubali uchezaji wake, ndipo alipomtaja Pacome na kumfafanua kwanini anamzikia.

“Kwanza napenda kumuita pacha wangu kwa sababu anavyojituma kwa bidii uwanjani, anavyowanyoosha wapinzani wetu, anatumia akili jinsi ya kutoa pasi na kukaba, lakini anaweka nywele blichi kama ninavyoweka mimi,” alisema Dora na kuongeza;

“Japo mimi ni shabiki wa Yanga lialia, lakini kwa ujumla napenda soka na michezo mingine, ndio maana nafahamu kwamba Pacome ni kati ya wachezaji bora nchini.”

Alisema mechi ambayo Pacome anaanzishwa anatumia muda mwingi kuiangalia, anajifunza jinsi ambavyo hakuna kazi inaweza ikafanyika kwa ufanisi bila kujituma.

“Sio lazima niwaangalie waigizaji wenzangu ndipo nijifunze vitu muhimu, bali anayefanya kazi nje na ninayoifanya, najifunza ili niwe bora zaidi,” alisema Dora anayefanya vizuri katika tamthilia ya Jua Kali.

Pamome anaichezea Yanga kwa msimu wa pili sasa akisajiliwa kutoka Asec Mimosas, rekodi zinaonyesha ameitumikia timu hiyo kwa dakika 1430 katika Ligi kuptia mechi 23 msimu uliopita akifunga mabao saba na asisti nne, huku mashuti 20 aliyopita yakilenga langio na 15 yakienda nje, huku akiifungia mabao matatu na asisti moja katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikiishia robo fainali.

Related Posts