Baada ya majadiliano makali kwenye kikao cha dharura, bodi ya Azam FC imefikia maamuzi ya kuliondoa benchi lote la ufundi chini ya kocha Yousouph Dabo.
Muda wowote kuanzia sasa taarifa rasmi itatoka na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa taratibu za kimikataba ili kila upande upate kinachostahili.
Dabo ataondoka na wasaidizi wake watano ambao ni kocha msaidizi Bruno Ferry (Ufaransa), kocha wa makipa Khalifa Babacar Fall (Senegal) kocha wa utimamu wa mwili Jean Laurent Geronimi (Ufaransa), mchambuzi wa video na wapinzani Ibrahim Diop (Senegal) na mchua misuli Ebrima Saine (Gambia).
Kuondoka kwa Dabo kunahitimisha mwaka mmoja wa utumishi wake ndani ya klabu hiyo, ulianza msimu uliopita.
Rekodi za Dabo akiwa na Azam FC
2. Kombe la Shirikisho la CRDB
3. Kombe la Shirikisho la CAF
Awali kocha huyo raia wa Senegal aliigawa bodi ya klabu juu ya hatima yake, baadhi ya wakurugenzi wakitaka aondolewe na wengine wakitaka abaki wakiamini anastahili kupewa muda.
Mgawanyiko ulianza baada ya kipigo cha 4-1 kutoka kwa Yanga, kwenye fainali ya ngao ya jamii, Agosti 11.
Baadhi ya wajumbe walikerwa, siyo tu na matokeo, bali namna timu ilivyocheza.
Wakamuita Dabo mwenyewe kwenye kikao cha dharura awaeleze kwanini aliamua kubadili mfumo wa uchezaji kutoka mabeki wa nne kama ilivyozoeleka hadi mabeki watatu siku hiyo?
Hoja ya msingi kwenye swali hili ilikuwa kocha anabadilishaje mbinu ya uchezaji dhidi ya timu kubwa na bora kama Yanga bila kuifanyia kazi.
Ifahamike kwamba wakurugenzi wa Azam FC walinunua kamera maalumu za kuonesha ‘LIVE’ mazoezi ya Azam FC kila inapofanya.
Kwa hiyo wamekuwa wakiyaona mazoezi ya timu hiyo siku zote, na hawakuwahi kuona akifundisha mfumo huo.
Dabo akasema aliujaribu mfumo huo kama maandalizi ya kuwakabili Pyramids kwa sababu akitaka autumie watakapokutana nao kwenye ligi ya mabingwa endapo watawatoa Pyramids.
Jibu hili halikuwafurahisha ‘mabosi’ hata kidogo na wakaanza kumuona mbabaishaji.
Ikaja mechi ya ligi ya mabingwa dhidi ya APR, hasa mchezo wa marudiano kule Kigali.Baada ya kipigo cha 2-0, wale wajumbe wa bodi waliotaka aondolewe tangu awali wakalipuka tena kwa hasira, safari hii wa kutumia nguvu zaidi.
Bahati mbaya kwao ni kwamba mwenyekiti wa bodi, Abubakar Bakhresa, alikuwepo Kigali na baada ya mechi aliingia chumba cha kuvalia cha wachezaji na wakuwapa pole na akaweka wazi kwamba bodi inamuunga mkono kocha Dabo na hatofukuzwa.
Abubakar Bakhresa ndiyo mtu pekee kwenye bodi ya klabu aliyekuwa akitaka kocha azidi kupewa muda.
Wajumbe wengine kama mdogo wake, Yusuf Bakhresa, ambaye ndiye aliyemleta kocha huyo, alishamkataa tangu msimu uliopita baada ya kutolewa na Bahir Dar ya Ethiopia kwenye Kombe la Shirikisho.
Kama maamuzi yangekuwa ya Yusuf peke yake, Dabo angekuwa ameshaondoka tangu Septemba mwaka 2023.
Lakini wajumbe wengine kama mwenyekiti wa bodi Abubakar Bakhresa na kaka yao Omar Bakhresa, pamoja na baba yao mdogo Jamal Bakhresa maarufu kama Bui, wakakubaliana kwamba wampe muda.
Lakini baada ya fainali ya ngapi ya jamii, Omar akaungana na Yusuf huku Jamal akiwa katikati…Abubakar akasimama na kocha.
Na hata baada ya mechi ya Kigali, wakati Abubakar anaingia kwenye chumba cha kuvalia, aliongozana na Jamal, wakiwa na msimamo mmoja kwamba kocha aendelee.
Lakini presha ya Omar na Yusuf ikawa kubwa baada ya hapo, hasa kiwango kibovu dhidi ya JKT Tanzania ndicho kilichowapa nguvu.
Wakaitisha kikao cha dharura usiku wa Ijumaa, Agosti 30 na kufikia muafaka kwamba IMETOSHA.