Mwenyekiti wa mtaa apiga magoti kuwaomba msamaha wananchi

Mwanza. Katika hali isiyo ya kawaida, mwenyekiti wa Mtaa wa California uliopo katika kata ya Nyegezi jijini Mwanza, Fadhili Nassoro amewapigia magoti wakazi wa mtaa huo, akiwaomba msamaha kwa makosa aliyowafanyia kwa kujua ama kutojua wakati wa uongozi wake.

Nassoro amechukua hatua hiyo Agosti 30, 2024 ikiwa imesalia miezi mitatu ya kukabidhi muhuri wa ofisi ya mtaa huo akisubiri uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajia kufanyika Novemba 27, 2024.

Imezoeleka wagombea wa nafasi za uongozi ndiyo wamekuwa wakipiga magoti kuomba kura kwa wananchi, lakini kwa Nassoro imekuwa tofauti, amepiga magoti kuomba radhi kwa wananchi kwa mambo mabaya aliyoyafanya wakati wa uongozi wake.

Akizungumza na Mwananchi, Nassoro amesema ameamua kuwapigia magoti na kuomba msamaha wananchi wake kwa kuwa  wakati mwingine kwenye uongozi kuna kuwakosea watu bila kujua.

“Mimi kama mwenyekiti wa mtaa, kwa sababu tunaenda kukabidhi mihuri yetu na kustaafu muda si mrefu, kupitia mkutano wangu mkuu wa mwisho wa mtaa nimepiga magoti kuwaomba msamaha wananchi wangu pale  nilipowakosea. Pia, namshukuru Mungu wananchi walikubali kunisamehe na mimi nimewasamehe kwa moyo mmoja,” amesema Nassoro.

Ameongeza: “Lengo ni kutembea kwa pamoja tumalize pamoja ili tutakapoanza Mungu akitujaalia tuanze kwa pamoja. Kwa haraka haraka sioni kama kuna jambo nilikuwa nimewakosea lakini natambua kwamba katika kuongoza wanadamu kuna sehemu unaweza kuwakosea kwa kujua au kutojua. Kwa hiyo, kama kuna sehemu niliwakosea kwa kutojua ndio maana niliamua kupiga magoti na kuwaomba msamaha.”

Amesema katika uongozi wake, bila kuvunja taratibu za kisheria, serikali ya Mtaa wa Califonia imeendelea kusikiliza kero kwa wananchi na kufanya mikutano na vikao vya ndani ili kuboresha maendeleo ya mtaa, huku akiwaomba wananchi kuongeza ushirikiano katika jitihada za maendeleo ya kulijenga Taifa.

“Tumefanikiwa kujenga ofisi ya serikali ya mtaa, mitaro na kujenga barabara ya kiwango cha mawe ili kuhimili adha za mvua kubwa zinazonyesha katika kipindi cha masika ambazo zinachangia uharibifu wa mazingira,” amesema Nassoro.

Baada ya mwenyekiti huyo kuomba msamaha, wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo walianza kuongea kwa sauti ya juu wakimwambia wamemsamehe kwa kuwa alijitoa hasa kwenye ulinzi shirikishi katika mtaa huo.

“Tumeibiwa sana kipindi cha nyuma, tulikuwa hatulali, wizi ulikuwa umekithiri, hata ukiacha nguo nje vibaka wanabeba, mwenyekiti amejikita kwenye ulinzi akipambana na vibaka kwa sababu stendi ipo karibu na inabeba watu wa hulka tofauti. Hivyo, tunaomba pia aweke jitihada zaidi katika maboresho ya ujenzi wa barabara za mtaa,” amesema mkazi wa mtaa huo, Anna Ngowi.

Mkazi mwingine wa mtaa huo, Yassin Suleimani amempongeza mwenyekiti huyo kwa jitihada za kukabiliana na changamoto katika uongozi wake, huku akiomba Serikali kushirikiana na wananchi kukamilisha ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa, ambayo wamefanya jitihada za kuchangishana fedha kwa ajili ya ujenzi huo.

Related Posts