Arusha. Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza, imewaachia huru Fikiri Kalamji na Samwel Kalamji, waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mama yao mzazi, Pili Ndulu ili warithi mali zilizoachwa na baba yao.
Fikiri na Samwel walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Disemba 24, 2020, ambapo walidaiwa kumuua mama yao kwa kutafuta watu wanaojulikana kama ‘wakata mapanga’ kufanya kitendo hicho cha kinyama.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama wa Rufani, Rehema Mkuye, Ignas Kitusi na Abdul-Hakim Ameir Issa, walisikiliza rufaa hiyo namba 163 ya mwaka 2021 na kutoa uamuzi huo Agosti 21, 2024, katika vikao vyake vilivyoketi Mwanza.
Majaji hao walifikia uamuzi huo wa kuwaachia Fikiri na Samwel baada ya kukubaliana kuwa maelezo ya onyo ya warufani hao yalikubaliwa kimakosa hivyo kuyafuta na baada ya kufuta kukakosekana ushahidi mwingine wa kuthibitisha kosa hilo.
Kutokana na dosari hiyo ya kisheria, majaji hao baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, walifuta hukumu iliyotolewa dhidi ya Fikiri na Samwel na kuamuru waachiliwe huru.
Awali Fikiri na Samwel walifikishwa Mahakama Kuu Masijala ya Geita, kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa Aprili 24, 2014 saa mbili usiku katika Kijiji cha Butegolumasa wilayani Chato mkoani Geita, walimuua mama yao Pili.
Awali baba yao alifariki Machi 2014, na kwa mujibu wa upande wa mashtaka, ilidaiwa baada ya kifo cha baba wa warufani walitaka kuchukua mali alizoacha baba yao na kuwa waligundua mama yao ambaye bado alikuwa hai, walimuona ni kikwazo.
Ilidaiwa vijana hao walipanga mpango wa kutaka mama yao auawe kwa kutafuta watu wanaojulikana kama “wakata mapanga” kufanya kazi hiyo na kuwa siku ya tukio, mama yao alivamiwa nyumbani kwake na kukatwa katwa hadi kufa.
Tukio hilo liliripotiwa polisi na baada ya uchunguzi kufanyika, ilidaiwa Fikiri na Samwel walihusika na tukio hilo, ambao walikamatwa.
Baada ya kukamatwa waliandika maelezo ya onyo ambayo wanadaiwa kukiri kumuua mama yao na walipofikishwa mahakamani walikana kutenda kosa hilo.
Fikiri alikana kumuua mama yake pamoja na kuuza ng’ombe ili kupata fedha za kuwalipa waliotenda tukio hilo na kuwa Mei 3, 2014 alipigiwa simu na kuitwa kituo cha polisi akituhumiwa kutenda kosa hilo.
Katika mahakama hiyo, Fikiri na Samwel walitiwa hatiani kwa msingi wa maelezo yao ya onyo ambayo yalikuwa ni kielelezo cha pili na nne, japokuwa mahakama ilikiri kwamba taarifa hizo zilikuwa na dosari ila ilitegemea maelezo hayo kwani iliamini warufani walieleza ukweli.
Fikiri na Samwel, waliwakilishwa na mawakili Constantine Mutalemwa na Geofrey Kange, ambapo walikuwa na hoja tatu za rufaa.
Hoja za Samwel zilikuwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, aliyeongezewa mamlaka ya kisheria kusikiliza shauri hilo la mauaji, alikosea kisheria kumtia hatiani kwa kutegemea maelezo ya onyo, ambayo yalipatikana kinyume cha sheria na kupokelewa kimakosa.
Nyingine ni hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani kwa kutegemea maelezo ya onyo ambayo hayajathibitishwa na Mahakama kukosea kisheria, kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kimazingira uliotolewa na upande wa mashtaka kuthibitisha shauri hilo pasipo shaka.
Kuhusu Fikiri, alidai Mahakama ilikosea kumtia hatiani kwa kuzingatia maelezo ya onyo yaliyorekodiwa kinyume na kifungu cha 57 na 58 cha Sheria ya Mwenendo ya Makosa ya Jinai (CPA).
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Castuce Ndamugoba.
Wakili Mutalemwa alidai wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, uwasilishwaji wa maelezo ya onyo ya Fikiri yalipingwa kwa kukiuka vifungu tajwa hapo juu na kuwa mshtakiwa hakupewa haki za kisheria.
Wakili huyo alidai kuwa suluhisho la dosari hiyo ni kufutwa kwa kielelezo hicho cha pili na kuongeza ikifutwa, hukumu ya Fikiri itatokana na maelezo ya onyo ya Samwel ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 33 (2) cha Sheria ya Ushahidi, mtuhumiwa hawezi kutiwa hatiani kwa kukiri tu mshitakiwa mwenzake bila ya uthibitisho.
Alidai maelezo hayo ya Samwel yaligubikwa na makosa na kudai yalichukuliwa kinyume na kifungu cha 58 cha CPA kwa madai kuwa askari polisi aliyerekodi hakutekeleza wajibu wake wa kumueleza Samwel haki za mtuhumiwa ikiwemo kumuuliza kama yuko tayari kutoa maelezo yake.
Wakili huyo alihitimisha hoja yake kwa kueleza iwapo maelezo hayo ya onyo yatafutwa, hakuna ushahidi mwingine wa kuthibitisha hukumu hiyo na kuomba mahakama ikubali rufaa hiyo, kufuta hukumu na kutengua adhabu.
Naye Wakili Kange, alikubaliana na hoja zilizowasilishwa na Wakili Mutalemwa na kueleza mahakama iliyosikiliza kesi hiyo, ilikiri kuwa maelezo ya onyo ya Samwel yalikumbwa na kasoro kutokana na kutokuwa na uhakika wa wakati mrufani huyo alipokamatwa.
Alidai kuwa kutokuwa na uhakika kunapaswa kutafsiriwa kuwa maelezo hayo ya onyo, yalirekodiwa kinyume na sheria kwani mtuhumiwa anapaswa kuandika maelezo ndani ya saa nne baada ya kukamatwa ila Samwel alikamatwa Mei 3, 2014 ila alihojiwa Mei 8, 2014.
Mbali na hayo, wakili aliielekeza mahakama ukurasa wa 180 wa kumbukumbu za rufaa inayoonyesha, Samwel aliulizwa ikiwa anahitaji mtu kuwepo wakati wa kurekodi maelezo yake na alijibu kuwa hataki, ila katika maelezo hayo inaonyesha Geofrey alisaini kama shahidi.
Wakili huyo aliiomba mahakama kufuta maelezo hayo ya onyo na kuongeza sababu nyingine ni kuwa maelezo hayo ya onyo hayakuthibitishwa na kuwa yanapaswa kuthibitishwa huku akirejea mashauri mbalimbali.
Wakili Ndamugoba, alianza kwa kueleza hapingani na rufaa hiyo na kukubali yale yaliyowasilishwa na mawakili wa warufani na kudai walitiwa hatiani kwa msingi wa maelezo ambayo yalikuwa na upungufu ambao unafanya thamani yao ya ushahidi kutiliwa shaka.
Alidai haikuelezwa ni lini warufani hao walikamatwa au kufikishwa vituo vya polisi, alikuwa na maoni kuwa kushindwa kufahamu muda wa kukamatwa warufani kunaleta shaka iwapo taarifa zao zilirekodiwa ndani ya muda au la.
Wakili huyo alidai maelezo ya Samwel ambayo yalirekodiwa na Sajenti Bahati (aliyefariki), yaliwasilishwa mahakama na shahidi mwingine baada ya kutoa notisi chini ya kifungu cha 289 (1) (2) na (3) cha CPA ambacho hakikutumika kwa hilo.
Ilidaiwa kuwa kifungu sahihi ni kifungu cha 34 B (2) (a) hadi (e) cha Sheria ya Ushahidi na kusisitiza mbali na Samwel kutopewa nafasi ya kupinga kutolewa kwake, hakimu aliyekuwa akisikiliza hakufanya uamuzi wowote juu yake na kuwa shahidi aliyetoa hakuwa na uwezo wa kuitoa mahakamani hapo.
Baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote na kupitia mwenendo wa shauri hilo, Jaji Mkuye, alieleza kuwa uamuzi wa kutiwa hatiani kwa Fikiri na Samwel ulitegemea maelezo yao ya onyo ,ambayo mawakili wa pande zote mbili wameeleza maelezo hayo yana upungufu wa kisheria.
Jaji Mkuye, amesema kuhusu kutofuata masharti ya kifungu cha 50, 51, 57 na 58 cha CPA, wanakubaliana na mawakili wote kuwa vifungu tajwa havikuzingatiwa.
“Kwa kuzingatia mamlaka zilizotajwa hapo juu katika kesi hii, tunaona kwamba ukiukwaji wa kutofuata kifungu cha 57 na 58 cha CPA ulikuwa mbaya na ulidhoofisha maelezo ya warufai na hivyo yanafutwa,” amesema Jaji Mkuye
Baada ya kuchambua hoja zote, majaji hao waliruhusu rufaa hiyo, kufuta hukumu iliyotolewa dhidi ya Fikiri na Samwel na kuweka kando hukumu zilizotolewa dhidi yao na kuamuru waachiwe huru.
“Kwa ukiukaji huu tunakubaliana na mawakili wote kwamba taarifa zote mbili za maelezo ya onyo zilikubaliwa kimakosa na kwa hivyo zinastahili kufutwa kama tunavyofanya na kama ilivyosemwa ikiwa taarifa hizo mbili zitafutwa, hakuna ushahidi mwingine wa kudumisha hukumu hiyo,” amesema Jaji Mkuye.