Sababu mashindano ya Quran kwa wanawake kufanyika Tanzania

Dar es Salaam. Haiba ya uadilifu, kupenda haki na usawa aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan, imetajwa kuchochea Tanzania ichaguliwe kuwa mwenyeji wa mashindano ya kwanza ya Quran kwa wanawake duniani.

Mashindano hayo yamehusisha washiriki kutoka mataifa 11 duniani, ni mara ya kwanza kufanyika na Tanzania imekuwa mwenyeji wake.

Hayo yameelezwa leo, Jumamosi Agosti 31, 2024 na Mufti  wa Tanzania, Sheikh Abubakar Bin Zubeir, alipohutubia katika mashindano hayo.

Amesema heshima iliyopata Tanzania kuwa mwenyeji wa kwanza wa mashindano hayo, imechochewa na haiba ya Rais Samia.

“Heshima ya mwanamke ni kubwa katika Uislamu na imekuwa heshima kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kwanza wa mashindano haya. Uamuzi huu umeangalia uadilifu, haki, usawa na wema wa Rais Samia,” amesema.

Katika hotuba yake, amemwomba Rais Samia ayalee mashindano hayo, akisema yanamhusu.

“Katika Quran, Msahafu mzima, kuna sura ya wanawake. Hatujapata bahati sisi wanaume Quran kuwa na sura ya wanaume,” ameeleza.

Si hivyo tu, amesema wanawake ni kundi lililotajwa zaidi katika Quran, jambo linalothibitisha, namna  jinsi hiyo ilivyopewa kipaumbele katika Uislamu.

Pia amezungumzia maadili na tabia njema, akisema kwa sasa yamevunjika.

“Leo kumetokea matatizo ya mmomonyoko wa maadili na ikatokea wanaoharibikiwa zaidi ni wanawake. Sasa hivi anaweza akafika mtu akamjibu mtu mzima vibaya, kumjibu mama yake vibaya, huku kote ni katika kukosa maadili,” amesema.

Amesema kuharibika kwa maadili ndiko kunakowafanya watu wasiheshimiane na kumsababisha aandike kitabu chenye maudhui ya maadili.

Awali, Akitoa taarifa ya mashindano hayo, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma amesema nchi 11 duniani zilizoingia fainali zimeshiriki  mashindano hayo.

Amezitaja nchi hizo kuwa Tanzania, Msumbiji, Sudan, Algeria, Jordan, Saud Arabia, Kuwait, Indonesia, Marekani, Ujerumani na Russia.

Kufanyika kwa mashindano hayo amesema kumelenga kuonyesha nafasi ya mwanamke kama ambavyo Uislamu umelijengea kundi la jinsi hiyo mazingira bora yanayohakikisha usalama, amani na haki.

“Tutakubaliana na ukweli kwamba, kumuelimisha mwanamke mmoja ni sawa na kuelimisha jamii, kutokana na nafasi yake katika kulea,” amesema.

Katika mashindano hayo yenye kaulimbiu ya ‘Mama ni Mlezi’, Mruma amesema hatua ya Tanzania kuwa na Rais mwanamke ndiyo iliyoifanya iwe mwenyeji wa tukio hilo.

“Ni nchi chache ambazo zina viongozi wanawake ndiyo maana jina la Rais Samia limekuwa nuru inayong’aa,” amesema.

Sababu nyingine zilizoifanya Tanzania iwe mwenyeji, amesema ni amani, mshikamano na ukarimu wa Watanzania.

Ameeleza tukio hilo ni fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na mataifa mbalimbali yaliyofika nchini na kwamba, kuna makubaliano ya ushirikiano kati ya Bakwata na taasisi ya kimataifa ya Muslim World Leage.

“Wito wetu ni kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake, ukatili wa kijinsia, unyanyasaji ndani ya jamii na kujenga maadili mema,” amesema.

Katika mashindano hayo, amesema washindi watatu watapatiwa tiketi ya kwenda Umra, huku mshindi wa kwanza akitunukiwa zawadi ya gari.

Related Posts