-Shamsa Ford alamba dili la ubalozi
Kiwanda cha YLM Food Company Ltd, kilichopo Kiwalani, kinachozalisha karanga za YY, kinatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara, wauzaji, na watu waliohitaji ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 31, 2024 Jijini Dar es Salaam, wakati wakimtangaza balozi wao mpya Shamsa Ford, Meneja wa kampuni hiyo, Christopher Godfrey, ameeleza kuwa zaidi ya Milioni 300 zimewekezwa katika kiwanda hicho, na hii ni dalili ya kuimarika kwa sekta ya viwanda nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Mi Yuiing ameleza kuwa uwekezaji huu umechochewa na fursa zilizotokana na ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini China, ambayo ilitokea kwamba Tanzania ina uwezo wa kuvutia wawekezaji.
“Uwekezaji huu sio tu kwa ajili ya uzalishaji wa karanga, bali pia unatoa nafasi za ajira kwa vijana zaidi ya 20 mpaka sasa, huku tukitarajia kutoa fursa zaidi kwa watu wengine”. Amesema
Kwa upande wake Balozi wa YY Karanga, Shamsa Ford, amewataka wafanyabiashara na mawakala kuchangamkia fursa hii ili kuongeza kipato chao na pia amewahakikishia wananchi kuhusu ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
“Kiwanda hiki kinatoa fursa nzuri kwa watanzania kujiajiri, kupata ajira, na kukuza uchumi wa eneo husika. Kwa wale wanaotafuta fursa za biashara, uwekezaji huu ni hatua nzuri ya kuweza kujiingizia kipato kupitia kuuza na kusambaza karanga”. Amesema