Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Viktor Yermolaev, mkuu wa kitengo cha wanamgambo kinachojulikana kwa jina la Medvedi (Bears) nchini Urusi na Bear Brigade huko Magharibi, amesema wapiganaji wake wengi wameondoka Burkina Faso, huku wachache tu wakisalia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Ukraine mapema mwezi huu ilianzisha uvamizi ambao haujawahi kushuhudiwa katika eneo la Kursk magharibi mwa Urusi, na kuongeza ari mpya katika vita vya zaidi ya miaka miwili vilivyoanza Februari 2022 na uvamizi wa Moscow dhidi ya jirani yake.
“Tunaona kwamba walichagua njia ya vita”
Kundi la The Bear Brigade ni mojawapo ya makundi kadhaa ya mamluki yaliyoibuka katika miaka ya hivi karibuni pamoja na Wagner Group la marehemu Yevgeny Prigozhin. Wachambuzi wanasema makundi hayo yana uhusiano wa karibu na serikali ya Moscow.
“Tulidhani Waukraine walitaka kumaliza vita hivi na kuketi kwenye meza ya mazungumzo, lakini baada ya kuingia katika eneo la Kursk tunaona kwamba walichagua njia ya vita, na vita ni kazi yetu,” alisema Yermolaev, ambaye pia anajulikana kwa jina la Jedi.
“Hakuna heshima kubwa kwa mpiganaji wa Urusi kuliko kulinda nchi yake. Hii ndiyo njia,” aliongeza Yermolaev, ambaye alisema amehudumu katika jeshi la anga la Urusi kwa miaka 15. Alisema sasa yuko Urusi lakini alikataa kutoa maelezo zaidi au kutaja ni wapiganaji wangapi wameondolewa nchini Burkina Faso.
Ushawishi wa Urusi katika ukanda wa Sahel
Mtandao wa Telegram wa kitengo hicho ulisema mapema wiki hii kwamba “kutokana na matukio ya hivi majuzi” kitengo hicho kilikuwa kikirejea Crimea, ambako ndio makao makuu yake.
Chanzo cha usalama cha Magharibi kiliiambia shirika la habari la AFP kwamba karibu wapiganaji mia moja wa kitengo cha kijeshi wameondoka Burkina Faso. Idara ya kijasusi ya nchi za Magharibi inaamini kwamba wapiganaji hao wamepewa jukumu hasa la kutoa usalama kwa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo Ibrahim Traore ambaye aliingia madarakani mwaka wa 2022.
Mfululizo wa mapinduzi katika nchi za Afrika Magharibi — nchini Mali mwaka 2021, Burkina Faso mwaka 2022 na Niger mwaka 2023 — umesababisha ongezeko kubwa la ushawishi wa Urusi, huku mamluki wa Urusi wakiitwa kusaidia serikali mpya. Viongozi wa mapinduzi nchini Burkina Faso waliwafukuza wanajeshi na wanadiplomasia kutoka kwa mtawala wa zamani wa kikoloni, Ufaransa na kugeukia Urusi kwaajili ya usaidizi wa kijeshi.
Aidha, Yermolaev alikataa kuzungumzia operesheni zao nchini Burkina Faso, lakini alisema kulikuwa na wapiganaji karibu 300 wa kikosi cha Bear Brigade katika nchi hiyo ya Kiafrika kabla ya uvamizi wa Kursk. “Baadhi wamesalia bila shaka, tuna kambi na mali, vifaa na risasi, hatupeleki vyote hivyo Urusi.”, alisema.
Athari katika vita dhidi ya ugaidi ?
Picha moja inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha Yermolaev akitabasamu na kuukumbatia mkono wa Traore. Yermolaev aliliambia shirika la AFP kuwa picha hiyo ilikuwa ya hivi majuzi, akisema “alipita ili kumuaga” Traore. Mwezi Juni, chanzo cha kidiplomasia cha Afrika kiliiambia AFP kwamba “ndege mbili zilizokuwa na wakufunzi wa Kirusi” ziliwasili nchini Burkina Faso kutoka nchi jirani ya Mali.
Jack Margolin, mtaalam huru wa makampuni binafsi ya kijeshi, alisema kuondoka kwa kundi hilo kutaathiri uwanja wa vita katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Kwa upande wake, Lou Osborn wa shirika la All Eyes on Wagner alikielezea kitengo hicho cha Bears Group kama “kundi la watu wa kujitolea” ambao wanachama wao walikuwa wametia saini mkataba na idara ya ujasusi ya kijeshi ya Urusi.
Operesheni za ulinzi wa usalama za Urusi barani Afrika sasa zinaratibiwa kupitia kikundi mwamvuli kinachojulikana kama Africa Corps.