Dar es Salaam. Mshiriki kutoka Algeria, ameibuka mshindi katika fainali za mashindano ya wanawake ya dunia ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Washindi wengine katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Agosti 31, 2024 ni wa pili kutoka Marekani, akifuatiwa na mwingine kutoka Jordan, Zanzibar na Tanzania Bara. Washindi wamepatiwa zawadi mbalimbali zikiwamo fedha.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi 11 na kufanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wilayani Temeke yameandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu Duniani, yakiwa na lengo la kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii.
Rais Samia Suluhu Hassan, aliyehudhuria mashindano hayo amesema taasisi za kidini zina wajibu wa kuandaa vijana katika misingi ya dini ili kuwa na maadili mema katika Taifa.
Kutokana na hilo, amezitaka taasisi hizo nchini, kubuni mbinu mpya zitakazowezesha kutoa elimu bora ya dini kwa vijana (wavulana na wasichana) na kina mama ili jamii iendelee kubaki katika misingi yake.
“Tutoe elimu ya dini kwa watoto wetu, lakini pia kwa kina mama ambao muda mwingi wanakaa na watoto, tuwaelimishe wote ili tuwe na misingi mizuri,” amesema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kila anapopata nafasi ya kuzungumza katika majukwaa ya kidini, anaeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha familia akisema huo ndiyo msingi wa Taifa na kwa asili wanawake wana nafasi kubwa katika ulezi wa familia bora.
“Kumlea mtoto wa kike katika misingi ya kiimani unakuwa unaandaa mwanamke au mama atakayeishi katika misingi hiyo, mtakubaliana na mimi watu wazima wenye misingi ya kutenda haki ni zao imara walilopitia katika makuzi yao,” amesema.
Amesema mtoto wa kike akipata elimu ya dini vizuri, siyo kuisoma Quran pekee bali aifahamu vema ikiwemo sura zake, basi ataweza kuwa mama na mwanamke bora wa baadaye.
Hata hivyo, amesema mkakati unakwenda sambamba na kuwalea watoto wa kiume vizuri kwa maadili, kama ilivyoelekezwa katika dini.
Rais Samia amesisitiza waumini wa Kiislamu wasiishie kuisoma tu Quran bali waelewe ina maelekezo gani, akisema katika kitabu hicho kitukufu, yapo majibu ya changamoto na njia zake zikifuatwa watu hawatapotea.
Sababu kufanyika Tanzania
Awali, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema heshima ya mwanamke ni kubwa katika Uiislamu ndiyo maana waandaji waliichagua Tanzania iandae mashindano hayo, akisema ni jambo kubwa ambalo Mungu ameliwezesha katika Taifa.
“Lakini sina shaka uchaguzi huu umetizama nchi yetu na ni kiongozi wake, mwadilifu, mpenda watu, mpenda usawa, mpenda haki walimuona mama yetu (Rais Samia) wakaamua wayaleta mashindano hapa Tanzania.
“Ni kweli kina mama wamewekwa mbele na Mungu, maana hata kwenye Quran ule msahafu mzima wenye sura 114, una sura ya wanawake pia, lakini wanaume hatukupata bahati kuwa na sura yenye jina letu,” amesema.
Akizungumzia mashindano hayo kufanyika Tanzania, Rais Samia amesema, “mashindano haya kufanyika hapa kulitokana pia na Tanzania kuendelea kukubalika kimataifa kutokana na kuwa na amani na utulivu, Watanzania tuendelea kuilinda.”
Katika hotuba yake, Sheikh Zubeir amesema Quran imekuja kufundisha maadili na tabia njema, lakini hivi sasa kuna changamoto ya mmomonyoko wa maadili na wanaolengwa zaidi kuharibiwa ni kina mama na vijana.
“Sasa mtu mzima anaweza kujibiwa vibaya, mtu haoni taabu kumsema baba au mama yake vibaya, huku ni kukosa maadili, Quran ambayo kina dada wameshindana hapa ndiyo inayotufundisha maadili mema.
“Tunatarajia tukitoka hapa tutakuwa tumejifunza maadili mema yanayotakiwa na Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume Muhammad (S.W.A) aliyoyafundisha,” amesema.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Nuhu Mruma amesema katika mashindano hayo yenye kaulimbiu ya ‘Mama ni Mlezi’, hatua ya Tanzania kuwa na Rais mwanamke ndiyo iliyoifanya iwe mwenyeji wa tukio hilo.
“Ni nchi chache ambazo zina viongozi wanawake, ndiyo maana jina la Rais Samia limekuwa nuru inayong’aa,” amesema.
Sheikh Mruma amesema mashindano hayo yameshirikisha Tanzania Bara na Zanzibar, Marekani, Algeria, Saudia Arabia, Msumbiji, Sudan, Jordan, Kuwait, Indonesia, Ujerumani na Russia.
Mashindano hayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa masihafu ya sauti iliyorekodiwa kwa wasomaji wa kuvutia wa Quran kutoka mataifa mbalimballi duniani.