Unguja. Wakati Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ikiwa katika hatua ya kwanza ya kutafuta maoni, timu kuu ya wataalamu imetaja mambo makuu matano yaliyojitokeza zaidi katika utoaji maoni na kuanza kuchakatwa.
Mkutano wa kwanza wa dira ya maoni ulifanyika Desemba 9, 2023 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Timu ya wataalamu inaendelea kukusanya maoni kwa njia ya makundi, mtu mmoja mmoja, viongozi wa dini na wanasiasa.
Kongamano la nne la Dira ya Taifa 2050 Kanda ya Zanzibar ambalo limejumuisha mikoa mitano ya Unguja na Pemba limefanyika leo Agosti 31, 2024 katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) kwenye Ukumbi wa Dk Mohamed Shein, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akitoa wasilisho kuhusu dira 2050 Tanzania tuitakayo, Mjumbe wa timu kuu ya timu ya kitaalamu ya dira hiyo, Dk Yahya Hamad Sheikh amesema maeneo hayo ni katika mageuzi ya kiuchumi, maendeleo ya watu, utawala bora, haki na ulinzi.
Mengine ni sayansi na teknolojia, huku mazingira na mabadiliko ya tabianchi pia ni miongoni mwa maoni yanayojitokeza zaidi.
Dk Yahya amesema katika uchambuzi wa maoni hayo jambo kubwa lililojitokeza wananchi walieleza namna wanavyotaka uchumi jumuishi, shirikishi, shindani na himilivu.
“Watu wanasema namna wanavyotaka kuona uchumi huu jumuishi, shirikishi na himilivu, unavyokwenda, haya ni maeneo ya kipaumbele ambayo yamebainika na kuanza kuchakatwa,” amesema.
Katika maendeleo ya watu na jamii amesema wananchi wengi wameeleza jinsi wanavyotaka huduma za afya ziboreshwe, upatikanaji wa majisafi na salama, lishe na makazi bora.
Maoni ya wengi walizungumzia masuala ya utawala bora, haki na ushirikishwaji na uwajibikaji kwa viongozi wakuu na wananchi wenyewe washirikishwe.
Katika sekta ya sayansi na teknolojia wananchi wengi wanasema fursa za sayansi na teknolojia zitumike kukuza uchumi na afya bora.
“Ikumbukwe miaka ijayo teknolojia itakuwa kubwa kwa hiyo ipo haja kujipanga na kwenda nayo ili isituache nyuma, Tanzania ijipange nayo,” amesema.
Kwa upande wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi amesema wanatamani kuona Tanzania inayojali na kuhifadhi mazingira yake.
“Tunaona jinsi mabadiliko ya tabianchi lilivyo janga la kidunia lakini sisi kama Taifa tunajipangaje kukabiliana na janga hilo,” amesema.
Khamis Ali, mkazi wa Nungwi amesema ifikapo mwaka 2050 anatamani kuona umeme hauzimiki tena nchini jambo ambalo litasaidia kuongeza uwekezaji na kuchochea maendeleo.
Siti Abasi Ali, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Zanzibar amesema katika dira hiyo, wanataka kuwaona wanawake wanaingia kwenye masuala ya uongozi kwa kuzingatia usawa wa asilimia 50 kwa 50 kwa vitendo.
“Tunataka tuone dira hii inatoa ufafanuzi, bado wanawake wanakufa na kupoteza maisha wakijifungua, tunataka tuwaone wanawake wakitumia simu zao kukuza biashara kwa matumizi ya gesi, maana pamoja na kutaka matumizi ya nishati safi lakini gharama ya kununua gesi ipo juu,” amesema.
Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar, Mohmed Makame amesema anatamani kuona vyuo vya amali vinaongezwa ili wanafunzi wengi wapate elimu, waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Khadija Ali ambaye ni mfanyabiashara amesema anatamani kupunguza masuala ya kodi ili kukuza biashara, huku ukiwekwa mkakati wa kuwa na mazao kwa ajili ya kujenga uchumi imara.
Mchango kama huo umetolewa na Mbunge wa Afrika Mashariki, Machano Ali Machano ambaye amesema ifikapo mwaka 2050 Tanzania inapaswa kuwa ya viwanda na itegemewe na mataifa mengine.
“Iwapo tukitaka kutoa ajira lazima tujenge viwanda na yale mazao yanayozalishwa ndani yatapata soko kwa hiyo Tanzania itaanza kutegemewa katika mazao na uzalishaji wa bidhaa,” amesema.
Fatma Ali, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Smail ametaka teknolojia itumike kukuza uchumi na kuwasaidia vijana kujiajiri.
Hamad Said, mdau wa utalii amesema, “tunataka kumuoana kijana anayejua historia ya nchi yake maana kwa sasa utalii imekuwa fursa lakini vijana wengi hawajui na wageni ukimdanganya unakuwa tayari umeshaharibu.”
Awali, akifungua kongamano hilo, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amesema wananchi wana wajibu wa kuona dira hiyo ni yao kwa hiyo watumie fursa kuishauri Serikali namna bora ya kuondoa changamoto zinazowakabili.
“Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 asilimia 77.5 ni watoto na vijana, kati ya hao ni kuanzia miaka 15 hadi 35 kwa hiyo lazima vijana waone umuhimu wa kutoa maoni,” amesema.