MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Maabad Maulid amesema jambo kubwa linalomuumiza kichwa ni kushindwa kufikisha angalau mabao 10 kwa msimu katika Ligi Kuu Bara tofauti na ilivyokuwa akicheza Ligi Kuu Zanzibar.
Nyota huyo aliifungia Coastal bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti dhidi ya KMC katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambao timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, Agosti 29, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maabad alisema endapo atakuwa fiti na ataendelea kupewa nafasi ya kucheza ndani ya timu hiyo atahakikisha angalau msimu huu afikishe mabao 10 katika ligi licha ya ushindani mkubwa uliopo.
“Huwezi kulinganisha ligi ya hapa na Zanzibar, ila nitapambana kufunga zaidi kila ambapo nitaendelea kupata nafasi ya kucheza. Bado sijaridhika na kiwango ambacho nimekionyesha, hivyo nina deni la kufanya kwa mashabiki zangu,” alisema mchezaji huyo.
Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022 akitokea KVZ FC ya Zanzibar ambapo aliibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo akianza msimu wa 2020-2021 mabao 17, kisha uliofuata wa 2021-2022 alifunga 21.
Licha ya rekodi hiyo bora, lakini tangu ajiunge na Coastal Union hajawahi kufikisha mabao matano Ligi Kuu Bara kwani msimu wa kwan-za wa 2022-2023 alifunga manne na uliopita matatu.