Bunda. Zaidi ya nyumba 55 za wakazi wa Kijiji cha Salama A wilayani Bunda, Mkoa wa Mara zimeezuliwa na kubomolewa na mvua iliyoambatana na upepo mkali hali iliyosababisha wakazi zaidi ya 150 kukosa makazi.
Pia upepo huo umeezua na kubomoa madarasa sita na nyumba mbili za walimu katika Shule ya Msingi Salama A na B katika kijiji hicho.
Akizungumza kijijini hapo leo Agosti 31, 2024, Diwani wa Salama, Emmanuel Makoba amesema tukio hilo limetokea Agosti 29,2024 majira ya jioni na kwamba hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea kutokana na tukio hilo.
Amesema kutokana na hali hiyo wakazi hao hivi sasa wanalazimika kijihifadhi kwa ndugu, rafiki na jamaa baada ya nyumba na mali walizokuwa nazo kuharibiwa.
“Wakazi hawa wanaishi kwa ndugu, jamaa na marafiki kwani kwa sasa hawana vyakula na mahali pa kulala kwa sababu vyakula vyote vililowanishwa na maji na mali zingine kuharibiwa baada ya paa kuezuliwa na nyumba kubomoka,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Salama B, Daudi Mazanginza amesema shule hizo mbili zenye jumla ya wanafunzi 1,401 zilikuwa na upungufu wa madarasa 12 kabla ya tukio hilo na kwamba kutokana na tukio hali ya upungufu wa madarsa imezidi kuwa mbaya.
“Hapa kila shule ina madarasa matano hivyo ni wastani wa wanafunzi 100 kila darasa kwahiyo kwa tukio hili ina maana hali itakuwa mbaya zaidi,” amesema
Amefafanua kuwa katika tukio hilo madarasa manne yaliezuliwa na upepo huku mawili yakipata nyufa kubwa hali iliyosababisha wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda vijiji kuelekeza yabomolewe kwani hayafai tena kwa matumizi.
Mkazi wa Kijiji cha Salama, Ngese Makoba amesema kwa ujumla miundombinu ya majengo katika shule hiyo ni mibovu na kuiomba Serikali kuangalia namna ya kusaidia ili shule hiyo iweze kujengwa upya.
“Tumeambiwa na wataalamu kubomoa madarasa mawili wakisema hayafai tena kwa matumizi, lakini ukweli ni kuwa madarasa yote hayafai kutumika yanahatarisha maisha ya wanafunzi na walimu tunaomba yabomolewe na kujengwa upya,” amesema Makoba
Mukaka Nyabunga amesema shule hiyo inakabiliwa na uchakavu mkubwa wa madarasa hivyo kuhitaji maboresho makubwa kutokana na shule kuwa na miaka takriban 60 tangu kujengwa.