Mbeya. Wakati Tanzania ikitarajia kufanya uchaguzi mkuu mwakani, Mbunge Viti Maalum, Sophia Mwanagenda amewataka wanaume kujifungia ndani ili waonyeshwe uwezo wa kuongoza kutoka kwa wanawake.
Mwakagenda ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 31,2024 mara baada ya kushiriki mashindano ya mapishi maarufu kama “Tulia Cooking Festival 2024” yaliyohusisha baba na mama lishe 1,000 yaliyofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini hapa .
Kauli ya Mwakagenda iliibua shangwe kwa mamia ya wananchi walioshiriki wakiwemo viongozi wa CCM wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM Taifa NEC Mkoa wa Mbeya , Ndele Mwaselela.
“Tunataka kuionyesha dunia kama wanawake tuna uwezo wa kuongoza nchi, tunao viongozi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na Spika mstaafu, Anna Makinda ambao wamefanya vizuri katika kuliongoza Taifa,” amesema Mwakagenda.
Amesema wakati wakielekea katika chaguzi zijazo umefika wakati wanaume wakae pembeni, wajifungie ili wanawake waonyeshe uwezo wa kugombea nafasi za uongozi na kuliongoza Taifa na nchi kwa ujumla na sio familia pekee.
Amesema miaka ya nyuma walijulikana wana kazi ya kupika na sio kugombea uongozi, sasa wanataka kuonyesha kama na wao wana uwezo wa kuongoza na kufanya vizuri.
“Tumeona hapa Dk Tulia ameandaa tukio hilo asilimia 90 ya wanawake wameshiriki, tunataka chaguzi zijazo mjitokeze kugombea ili kumuunga mkono “amesema Mwakagenda huku akishangiliwa.
Amesema licha ya kuwa mfuasi wa Chadema na kulala polisi, lakini 4R za Rais Samis Suluhu Hassan zimewaweka vizuri.
Kwa upande wake, Mwaselela amesema kama chama hawana muda wa kupoteza kumpa ridhaa mtu mwingine kugombea Mbeya mjini huku akimpongeza Mwakagenda kwa ushiriki wake katika mkusanyiko huo.
“Tutamlinda Dk Tulia Ackson kwa hali yoyote na kuhakikisha uchaguzi ujao anapata kura za kishindo ili aendelee kuwapigania wananchi wake kuleta maendeleo ya kweli kwa jimbo la Mbeya,” amesema