Dodoma. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amewataka watu kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, ili kujenga uchumi na sio kulalamika katika mitandao ya kijamii.
Dk Mwigulu ameyasema hayo leo Jumamosi Agosti 31, 2024 wakati akifungua mkutano kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sheria ya Ubia kati sekta Binafsi na mafunzo ya takwimu zinazozalishwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu.
“Fikiria kama kwenye ukandarasi umempa, kununua material (malighafi) zinazotakiwa katika ukandarasi ule amenunua kutoka nje ya nchi, halafu baada ya hapo dola zikiadimika mnaelekeza lawama serikalini. Kama kila kitu umewapa watu wakaondoka nacho sasa baada ya hapo itatoka wapi?” amehoji.
Amehoji dola zinatoka wapi kama kila zabuni unawapa wageni na kwenye nyaraka ya zabuni umeelekeza hata nondo na malighafi nyingine zipo Tanzania lakini umeelekeza zitoke nje ya nchi.
“Baada ya hapo vidola vyote tunavyokusanya vinaenda hapo halafu baada ya hapo unasema dola hazipo unauliza Serikali. Inatokea mimi naposti picha tu ya kijana wangu wa chipukizi na mmu-wish happy birthday (hongera kwa kumbukizi ya kuzaliwa) mnaanza kusema kameshiba dola zetu, amesema.
Amesema wameleta sheria lakini watu wamekuwa hawapendelei Taifa lao na kwamba ni vizuri watu wakaelewa vitu ambavyo ni vya mnyororo.
Ametaka Watanzania kutengeneza sekta binafsi ya Tanzania na kuwa hata wageni walikuja wakiwa wadogo ambapo kila kitu wamekipatia hapa nchini.
“Na wengine wamekuwa wakubwa kwa kuwatumia Watanzania kwa heshima tuliyojijengea hapa Tanzania tulitakiwa kuwa na kampuni kubwa zilizotapakaa nchini,” amesema.
Amewataka Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazozalishwa nje ya nchi zitumike pale ambapo hazipo hapa nchini.
Naye Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, amesema wamepata changamoto wakati wa utekelezaji wa mfumo mpya wa ununuzi wa NeST ikiwemo kasi ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa ‘Force account’.
Amesema wamekuwa na changamoto kubwa ya bei kupitia mfumo mpya wa ununuzi ambapo awali bei ya bidhaa zilitokana na thamani ya soko.
Mkutano huo uliwashirikisha wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mkoa, wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini.