Tabora. Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba nchini (TMDA) Kanda ya Magharibi, imefanikiwa kukamata dawa na vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani zaidi ya Sh150 katika kipindi cha kuanzia Januari 2023 hadi Agosti 2024.
Akizungumza na Mwananchi Agosti 30, Meneja wa kanda hiyo, Christopher Migoha amesema oparesheni zimekuwa zikifanyika kwa kushtukiza, jambo lililowafanya wanase dawa na vifaa tiba hivyo.
“Katika kipindi cha Januari 2023 hadi Agosti 2024, tumefanikiwa kukamata dawa na vifaatiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya zaidi ya Sh150 milioni na vifaa hivi tumevikamata wakati vinaingizwa nchini na vingine vikiwa tayari vimeanza kuuzwa kwenye maduka,” amesema na kuongeza:
“Operesheni tulizofanya zilihusisha mipaka ya Manyovu, Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma ambapo maeneo hayo yamepakana na nchi ya Burundi na huko tulifanikiwa kudhibiti uingizwaji wa dawa na vifaatiba kwa lengo la kuwalinda wananchi wetu na matumizi ya dawa zisizo na ubora,” amesema.
Hata hivyo, Migoha amewataka wakazi wa kanda hiyo kujenga tabia ya kupima magonjwa na kupewa dawa katika maeneo yanayotambulika, badala ya kununua dawa kiholela huku wengine wakipewa dawa ambazo hazina ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine, Migoha amesema mamlaka hiyo itaendelea kufanya ukaguzi kwa maduka na maeneo yote ambayo yanafanya biashara za dawa na vifaatiba ili kuhakiki vifaatiba na dawa zinazouzwa kama ni bora, na kwa wale ambao watakutwa na dawa pamoja na vifaatiba visivyo na ubora watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, daktari kutoka hospitali ya Nzega, Sarah Boniphace amesema dawa zinapoingizwa nchini zikiwa chini ya ubora zinaweza kusababisha madhara kwa binadamu, hivyo ni vyema wagonjwa kuchukua dawa maeneo yanayotambulika.
“Tumeshuhudia mara kadhaa shehena za dawa zikikamatwa zikiwa hazina ubora unaotakiwa ikiwa ni pamoja na vifaatiba.Kwenye mazingira kama haya tunawasihi wagonjwa wanapohisi kuumwa waende kupewa vipimo kisha wapate dawa maeneo yanayotambulika, ili kuondoa watu kutumia dawa ambazo hazina ubora.
Mrutu Saleh, mkazi wa Nzega ameiomba mamlaka hiyo kuongeza nguvu katika udhibiti wa ukamataji dawa na vifaa tiba ambavyo havina ubora ili kuwaokoa Watanzania.
“Imejengeka tabia ya watu wengi wanapohisi kuumwa wanaenda kununua dawa bila kupima, na wananunua dawa kwenye maduka ambayo wakati mwingine hayajasajiliwa kabisa hivyo mamlaka zinatakiwa kuongeza jitihada kudhibiti waingizaji na wasambazaji dawa ili kuepusha madhara kwa wananchi,” amesema.