Dar es Salaam. Hali ya kisiasa nchini na uteuzi wa mgombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki na maandalizi wa mkutano mkuu maalumu, ni miongoni mwa ajenda zinazotajwa kuchukua nafasi kwenye kikao cha Kamati Kuu Maalumu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotarajiwa kufanyika kesho Septemba Mosi, 2024.
Pia, ajenda nyingine inatajwa kuwa ni maandalizi ya kujaza nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho atakayechukua nafasi ya Abdulrahman Kinana ambaye alijiuzulu katika nafasi hiyo Julai 19, 2024.
Jana, Agosti 30, 2024, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari akieleza kwamba CCM kitakuwa na kikao cha Kamati Kuu Maalumu, kitakachofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 2, 2024, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kutolewa marekebisho leo kuwa kitafanyika kesho.
Pia, taarifa hiyo ya Makalla inaeleza kwamba kikao hicho cha Kamati Kuu, kitatanguliwa na kikao cha sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kinachofanyika Agosti 31, 2024, jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kinafanyika wakati matukio kadhaa yakiwa yametokea nchini na yanahitaji watu kukaa na kufanya uamuzi ili mambo mengine yaendelee.
Uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa Bunge hilo katika kundi la wanawake kupitia CCM, Dk Shongo Sedoyeka, kilichotokea Juni 13, 2024.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatakiwa kufanya uchaguzi mdogo wa mbunge ili kujaza nafasi hiyo kwa mujibu wa kanuni.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu ulifanyika kwa siku sita kuanzia Agosti 10 na kuhitimishwa Agosti 15, 2024.
Tayari wagombea 47 kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuwania nafasi moja ya ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu kikao hicho, Katibu wa zamani wa Kamati Maalumu, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Nao amesema kikao cha kamati kuu maalumu huitishwa kwa jambo maalumu ambalo linahitaji uamuzi.
“Kuna vikao vya kikatiba ambavyo vinakwenda kwa mujibu wa kalenda, halafu kuna vikao vya dharura au maalumu, kwa hiyo kikao hicho kimeitishwa kwa jambo maalumu, mimi na wewe hatulifahamu kwa sababu siyo waandaaji wa hivyo vikao,” amesema.
Hata hivyo, aliyekuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (Nec), Angelina Akilimali amesema kikao hicho kitajadili masuala mbalimbali yaliyojitokeza katikati ya kikao kimoja na kingine cha kamati kuu.
“Kwa kawaida kamati kuu inakaa mara moja kila mwisho wa mwezi, kikao cha Agosti kilishafanyika, kwa hiyo hiki kinakaa kwa ajili ya kujadili jambo maalumu linalohitaji kuamuliwa haraka,” amesema Akilimali.
Amesema licha ya kwamba ajenda za kikao hicho hazifahamiki, lakini kuna mambo yametokea siku zilizopita ambayo yanahitaji kufanyiwa uamuzi, miongoni mwa mambo hayo ni uteuzi wa mgombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki na maandalizi ya mkutano mkuu kwa ajili ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM – Tanzania Bara.
“Hicho kikao maalumu huwezi kujua wanajadili mambo gani kwa sababu kuna mambo mengi. Kuna uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
“Makamu Mwenyekiti alishajiuzulu, kwa hiyo lazima achaguliwe Makamu Mwenyekiti mwingine, huenda ni moja ya ajenda pia ili kuruhusu mkutano mkuu maalumu ufanyike, ndiyo maana unaitwa maalumu kutokana na ajenda zilizopo mezani,” amesema Akilimali.
Kada mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe, amebainisha kwamba moja ya mambo yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na hali ya kisiasa nchini kuelekea uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, natarajia jambo hilo litaibuka kwenye kikao hicho kwa sababu chama chetu kinatafuta ushindi na ili upate ushindi lazima mjadiliane namna ya kuwashawishi wananchi,” amesema kada huyo.
Wakati kikao hicho kikitarajiwa kufanyika, matarajio ya makada wengine wa chama hicho uteuzi wa atakayejaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara ambapo hadi sasa baadhi ya watu wanatajwa akiwemo mawaziri wakuu wastaafu, Mizengo Pinda na Frederick Sumaye, Abdallah Bulembo, Stephen Wasira.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Charles Gishuli amesema anadhani Pinda ndiyo anafaa Makamu Mwenyekiti kwa sababu amefanya kazi kubwa akiwa Naibu Waziri na Waziri Mkuu na sifa zake ni unyenyekevu na uadilifu.
“Hajawahi kuwa na kashfa ya ubadhirifu wa mali ya umma na anajua kuheshimu mamlaka yake, kazi ya makamu ni kuwa msaidizi wa mkuu wako, kazi ya usaidizi inahitaji unyenyekevu na heshima, sifa hizo Pinda anazo. Kwa unyenyekevu huo si rahisi kujiinua na kuasi mamlaka yake,” amesema.