Waliositisha masomo kwa ujauzito wasimulia machungu

Mwanza. Wasichana waliositisha elimu katika ngazi mbalimbali mkoani hapa, wameelezea changamoto wanazopitia ikiwemo unyanyapaa, kufukuzwa na kutolewa lugha chafu na ndugu zao.

Hata hivyo, wanafunzi hao sasa wamepata matumaini baada ya kurejea katika mfumo wa elimu baada ya kupata mafunzo ya ufundi stadi.

Wamesimulia machungu hayo leo Agosti 31, 2024 katika mahafali ya nane ya Chuo cha ufundi stadi cha Zawadi Initiative kilichopo Buzuruga jijini Mwanza.

Aisha Twaha aliyesitisha masomo kwa kupewa ujauzito akiwa darasa la saba, amesema baada ya kupewa mimba mbali na kukatishwa masomo, hata nyumbani kwao alifukuzwa na wazazi wake.

“Nilipata mimba nikiwa darasa la saba baada ya hapo nilifukuzwa shule, lakini pia hata wazazi wangu walichukia kupokea taarifa za kuwa nina mimba na wao wakanifukuza nyumbani.

“Nikaona sehemu pekee ya kukimbilia ni kwa dada yangu ambaye anaishi Mabatini Mwanza ambapo huko niliishi kwa zaidi ya miaka miwili,” amesema.

Amesema baada miaka miwili, alirudi nyumbani kuwaomba msamaha wazazi wake wakaendelea kuishi kama zamani.

“Wahenga wanasema ‘mtoto kwa mzazi hakui’ na mume wangu mpaka sasa ninaishi naye kwa sababu baada ya kutokea hilo alinichukua,” amesema Aisha.

Hata hivyo, matumaini yamerejea Februari mwaka huu baada ya kupata nafasi ya kujiunga na Chuo cha Ufundi kinachosimamiwa na Taasisi ya Zawadi Initiative, ambapo amesema kupitia ujuzi aliopata wa ufundi seremala na ujasiriamali, anaweza kurejesha matumaini ya mafanikio katika maisha yake.

“Matumaini yangu ni makubwa sana kwa sababu nilikuja sijui hata kunyonga cherehani, ila baada ya wiki mbili nikaweza kwa sasa naona mwanga wa kutimiza ndoto zangu natamani nije nifungue kampuni kubwa ya ushonaji nguo kwa ajili ya kujiingizia kipato,” amesema Aisha

Kwa upande wake, Aneth Masalu ambaye ni mkazi wa Nyashigwe Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, alikatisha masomo akiwa kidato cha tatu baada ya kupata ujauzito hali iliyomsababisha kutoweka nyumbani kwa kuhofia wazazi.

“Siku ya kwanza kugundua nina mimba nilishtuka sana na nikawa na hofu sana nikiwaza wazazi wangu watalipokeaje hili baada shuleni kujulikana kuwa nina mimba nilirudishwa nyumbani, ambapo napo nilikosa ujasiri wa kukaa pale nyumbani.

“Ikabidi nitoweke kwa muda pale nyumbani kwa muda wa wiki mbili, baada ya wazazi kuanza kunitafuta ndipo nilirudi nyumbani tukazingumza na kuyamaliza,” amesema.

Amewashauri wanajamii kutowatolea lugha za matusi mabinti wanaopata mimba wakiwa bado wanasoma, kwani ni kuwakatisha tamaa ya maisha.

Akizungumza katika mahafali hayo kwa njia ya mtandao Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Zawadi Initiative, Bupe Kyelu amesema, mbali na kusaidia mabinti wanaopata mimba wakiwa bado shuleni pia chuo hicho kinatoa mafunzo kwa wanawake wasio na kazi.

“Tunajisikia fahari ndani ya miaka minane tumewafikia wanawake 215 na hawa wa leo 75 jumla tutakuwa tumefikia 292 kati ya 300 ambao tulikuwa tunatarajia kuwafikia hiyo ni idadi kubwa ukilinganisha na udogo wa taasisi yenyewe,” amesema.

Amesema pia wanawafikia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira, ambapo malengo yao katika kipindi cha miaka 10 yalikuwa ni kuwafikia wanafunzi 500.

“Mpaka sasa tupo mwaka wa nane tumewafikia wanafunzi 1,075 katika Mkoa wa Mwanza,” amesema Kyelu

Ofisa Maendeleo Manispaa ya Ilemela, Fidelis Kiraryo akimwakilisha Msajili Msaidizi wa asasi zisizo za kiraia katika manispaa hiyo,  amewaomba wahitimu kuunda vikundi vitakavyowasaidia kuomba na kupewa mikopo kutoka serikalini ili kufikia malengo yao.

“Kwa walengwa wote ambao wamepewa mafunzo haya tunawaomba wakae kwenye vikundi ili Serikali iwawezeshe mabinti na wanawake hawa kupitia mikopo na fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na makundi maalumu,” amesema.

Related Posts