Lushoto. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Paul Kihwelo amehimiza kuimarishwa kwa mbinu za upelelezi wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori na misitu ili kupata ushahidi utakaowezesha haki itendeke kwa wenye hatia.
Jaji Kihwelo ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) mkoani Tanga, amesema hayo jana Aprili 29, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kundi la pili la awamu ya nne la wadau wa haki jinai zaidi ya 100 kuhusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori ukiwamo ujangili na makosa ya misitu, chuoni Lushoto.
Mafunzo hayo yatakayochukua wiki moja yanaendeshwa na IJA kwa ufadhili wa Taasisi ya PAMS Foundation inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori.
Washiriki wa mafunzo hayo ni majaji wa Mahakama Kuu, mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi wa ngazi mbalimbali kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Tanga.
“Mkusanyiko huu unasaidia sana kujadili changamoto, mfano kuna changamoto nyingi za kiupelelezi ambazo mwisho wa siku zinafanya makosa, kesi zinashindwa kufanikiwa au zinafutwa na wakati mwingine kushindwa kuthibitishwa,” amesema Jaji Kihwelo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Pams Foundation, Samson Kassala amesema taasisi yake hiyo imekuwa ikifadhili mafunzo hayo ili kuunga mkono vyombo vya haki jinai katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na misitu lengo ni kuona kizazi kijacho kinanufaika na rasilimali hizo.
“Tunawezesha mafunzo haya, lengo ni kuunga mkono juhudi za vyombo vya haki jinai na Serikali kwa ujumla katika kukabiliana na ujangili, tunapenda kuona rasilimali hizo zinarithishwa kwa kizazi kijacho ili nacho kinufaike kama tunavyonufaika sisi leo hii,” amesema Kassala.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo Ofisa Mhifadhi kutoka Mamlaka ya uhifadhi wa wanyama pori Tanzania (Tawa), Rutaga Kona amesema kuwa mafunzo hayo yatamsaidia kutanua wigo wa uelewa wa masuala haya ya wanyamapori kati ya vyombo vya ulinzi na vya sheria katika kushughulikia masuala ya ujangili na uharibifu wa misitu.
Wakili wa Serikali Mkoa wa Arusha Amanda Evansi Lushakuzi amesema, “kuna changamoto katika masuala ya ukamataji, katika masuala ya nyara zinapokuja kupekuliwa na kupelekwa kwa mkemia na mpaka kesi ije kupelekwa mahakamani.
“Hivyo changamoto zote hizo zitajadiliwa, tuone tutaziwekaje ili Mahakama pamoja na wapelelelezi wote tuwe kitu kimoja maana wapelelezi wao ndio wanaotengeneza kesi,” amesema Wakili Lushakuzi.