SIMBA ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu Bara ambayo ina taji lolote hadi sasa msimu huu, japo ukimweleza hilo shabiki wa Wekundu wa Msimbazi atakuona kama unamkebehi.
Lakini huo ndio ukweli. Ila kwanini wengi wanauchukulia poa? Ni kwa sababu wanasahau ukweli mzito kwamba Simba imetwaa mataji hayo mawili – Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano – kwa kuziangusha timu mbili bora za Tanzania na washindani wao wakuu katika mataji yote, Yanga na Azam.
Simba iliibwaga Yanga kwa penalti katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii ambayo kwa mara ya kwanza msimu huu imefanyika kwa mtindo wa mtoano ikishirikisha timu nne, Simba, Yanga, Azam na Singida Fountain Gate.
Na wekundu hao pia wakaifunga Azam FC 1-0 katika fainali ya Kombe la Muungano ambalo nalo mara hii kwa mara ya kwanza limefanyika kwa mtindo wa mtoano likishirikisha timu nne pia za Simba, Azam, KMKM na KVZ.
Simba ilicheza fainali ya Kombe la Muungano na Azam utadhani ilikuwa ikicheza dhidi ya timu ya mchangani.
Kama ingekuwa na wamaliziaji walio katika ubora pale mbele, ingeweza kushinda mechi ile kwa mabao zaidi ya matano.
Ndani ya dakika chache za mapema tu Simba ingeweza kuongoza kwa mabao mawili kama Willy Essomba Onana aliyebaki na kipa mara mbili angethibitisha kwamba yeye ni “mali” kwa kufunga nafasi zile zilizoonekana ni rahisi sana kwa mdunguaji wa ukweli.
Kipa wa kimataifa wa Sudan, Mohamed Mustafa, alikuwa katika ubora wake langoni mwa Azam akiokoa hatari zilizofululizana moja baada ya nyingine ikiwamo ya kichwa cha Kibu Denis kutokana na kona ya Saido Ntibazonkiza na kona nyingine kadhaa.
Simba ililishambulia lango za Azam mfululizo na ilikuwa ni mara chache sana kuwaona nyota wa timu ya Chamazi wakileta hatari langoni mwa Simba.
Kiufupi, fainali ya Kombe la Muungano ilikuwa ni mjumuisho wa tatizo la Simba la msimu mzima la kutobadili nafasi nyingi inazotengeneza na mashuti mengi inayopiga kwa wapinzani kuwa mabao.
Mfano mwingine hai ni mechi ya marudiano ya Kariakoo Dabi ambayo Wekundu wa Msimbazi walilala 2-1.
Hii ni mechi nyingine ambayo Simba ingeweza kushinda kama ingekuwa na wadunguaji walio katika ubora wao.
Yanga ilipiga mashuti saba mechi nzima, manne yalilenga lango na matatu yalienda nje, Simba ilipiga mashuti 10, manne yakilenga lango na sita yalienda nje.
Unaweza kuona hapo, Yanga katika mashuti manne yaliyolenga lango ilifunga mabao mawili lakini Simba ilifunga bao moja tu kati ya mashuti yake manne.
Hili ni tatizo la msimu mzima. Ni jambo ambalo limekuwa likitokea katika karibu kila mechi.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ingeweza kuwatoa mabingwa mara 11 wa Afrika, Al Ahly kama ingekuwa na wadunguaji walio katika ubora wao.
Hili jambo tumeshalisema hapa na kamwe hatutaacha kulirudia kwa sababu ni ugonjwa unaopaswa kutafutiwa tiba.
Katika mechi ya Dar, Simba ilitawala kila kitu isipokuwa mabao tu.
Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 62 dhidi ya 38 za Ahly, ikapiga mashuti 19 dhidi ya 5 ya Ahly. Mashuti ya Simba yaliyolenga lango yalikuwa 7 hapakuwa na bao na badala yake ikalala 1-0 kupitia kwa shuti pekee la Ahly lililolenga lango la Simba. Simba pia ilienda kutawala umiliki wa mpira hata kule Cairo katika mechi ya marudiano na Ahly ambayo badala yake Wekundu wa Msimbazi wakalala 2-0.
Hili ni tatizo ambalo linahitaji tiba.
Kule kwenye Ligi ya Mabingwa kiujumla, katika hatua ya makundi, Simba ndiyo timu iliyoshika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi nyingi zaidi za hatari ikitengeneza 19 nyuma ya Ahly iliyotengeneza nafasi 24. Kwa hali hii ni wazi kwamba tatizo la Simba ni umaliziaji kwa sababu kutawala mechi dhidi ya mabingwa wa Afrika nyumbani na ugenini sio jambo la kulichukulia poa na timu mbovu hauwezi kufanya hivi.
Kama unaamini zile propaganda kwamba Simba imekutana na Al Ahly iliyochoka, waulize TP Mazembe kilichowakuta pale Cairo katika nusu fainali wiki iliyopita. Walikimbizwa na wakala 3-0!
Kuondoka ghafla kusikotegemewa kwa kocha wao, Abdelhak Benchika hakika kutaifanya Simba irudi nyuma katika ndoto zile za kutisha Afrika.
Kwa sababu Benchikha ni kocha mwenye wasifu wa kocha wa kiwango cha juu kabisa Afrika na Simba kumpata ilikuwa ni kama kuokota dodo chini ya mnazi.
Kuamuacha aondoke kabla ya kumpa dirisha moja kubwa la uhamisho ili alitumie kuijenga timu kwa viwango vya kubeba mataji ya Afrika, ni pigo kubwa kwa Simba.
Kumpata kocha mwenye medali ya ubingwa wa Afrika kama wa hadhi ya Benchikha sio jambo rahisi, Ni lazima pesa zikutoke.
Kama tunachokisikia ni kweli kwamba kuondoka kwa kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Algeria kumechangiwa pia na ukubwa wa gharama kutokana na kuishi kwake hotelini huku akivuta mshahara wa zaidi ya Sh50 milioni kwa mwezi huku pia benchi lake likilipwa mishahara minono, basi Simba inatakiwa kukumbuka kwamba mambo mazuri ni gharama.
Kama ni kweli kwamba Simba imeona ni mzigo kumlipa pesa nyingi kocha huyo na benchi lake huku timu ikiwa haipo katika kupigania mataji makubwa na hivyo kuingia dili la kuachana naye kwa amani, basi tunaikumbusha kwamba kama iliweza kumlipa kwa miezi yote tangu alipotua mwishoni mwa mwaka jana, ingeweza kuvumilia mwezi mmoja uliobaki ili ahusike kwenye kuijenga timu katika dirisha kubwa lijalo la uhamisho.
Lakini kama ni kweli, kama tulivyofahamishwa, kwamba ni yeye aliyeomba kuondoka, sio mbaya sana hasa kama ilijaribu na kushindwa kumshawishi abaki hadi wakati wa usajili kwa sababu yeye ni kocha mkubwa na angeweza kuwavutia wachezaji wa kiwango cha juu.
Lakini maji yakimwagika hayazoleki. Benchikha ameshaondoka na kilichobaki Simba ni kuangalia mbele. Na katika mikakati ya kuirejesha ile Simba ya kutisha iliyotawala kwa kutwaa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-18 hadi 2020-21 na kucheza robo fainali za CAF mfululizo, iweke nguvu kubwa katika kununua wadunguaji wa ukweli. Ikiwapata watatu itapendeza kwa sababu maeneo mengine ya uwanja yanazungumzika!