Dk Nchimbi, Masoud wakwamisha mdahalo wa makatibu wakuu wa vyama

Dar es Salaam. Katika hali isiyotarajiwa, mdahalo uliopangwa kuwahusisha makatibu wakuu wa vyama vitano vya siasa nchini, umeshindwa kufanyika.

Mdahalo huo uliopangwa kurushwa kwenye kipindi cha Medani za Siasa cha kituo cha luninga cha Star TV jana Agosti 31, 2024 ulitarajiwa pia kumuhusisha Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ambaye hakutokea.

Kushindwa kufanyika kwake, kumetokana na kile kilichoelezwa na mtangazaji wa kipindi hicho, Edwin Odemba kuwa, Dk Nchimbi hakutokea eneo la mdahalo katika Ukumbi wa Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku pia Katibu Mkuu wa CUF, Ahmad Masoud ambaye yupo kwenye matibabu nje ya nchi, alituma mwakilishi.

Kuhusu Dk Nchimbi ambaye hakutuma mwakilishi, Mwananchi ilipomtafuta Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla kutaka kufahamu sababu hakupokea simu.

Hata hivyo, pamoja na kushindikana kufanyika kwa mdahalo wa viongozi hao, mada mbalimbali zilizopangwa zimejadiliwa na wahudhuriaji wa tukio hilo.

Akitangaza hatua ya mdahalo huo kutohusisha watendaji wakuu wa vyama, Odemba amesema kwa bahati mbaya na masikitiko Dk Nchimbi hatakuwepo katika mdahalo huo.

“Kwa kuwa nia yetu ni njema na tuliandaa mdahalo huu wa wazi, kwa nia ya wazi tunalaani vikali kitendo hiki kisichokuwa cha kiungwana kilichoendelea. Lakini tumesema mjadala huu lazima uendelee,” amesema huku akibubujikwa na machozi.

Baada ya Dk Nchimbi kutohudhuria, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alikataa kushiriki kwa kile alichoeleza hatafanya hivyo kama mtendaji mkuu wa CCM hatakuwepo.

Alisema hata Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu naye amesema hatashiriki kwa kuwa Mnyika amegomea hilo.

Alieleza hata Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Martha Chiomba naye amesema hatashiriki kwa sababu wenzake hawashiriki.

Baada ya kutangaza hilo, majadiliano ya mada zilizoandaliwa yaliendelea yakihusisha wahudhuriaji.

Related Posts