Wanaodaiwa kumteka aliyechoma picha ya Rais wataka Sh3 milioni

Mbeya. Zikiwa zimepita siku 30 tangu mkazi wa Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Shadrack Chaula kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, hatimaye wamemtaka baba mzazi wa kijana huyo kutoka Sh3 milioni ili wamwachie mwanawe.

Shadrack anadaiwa kutekwa na watu hao Agosti 2, 2024 zikiwa zimepita siku 20 tangu alipotoka Gereza la Ruanda mkoani Mbeya, alipokuwa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya Sh5 milioni.

Leo Jumapili, Septemba 1, 2024, Yusuph Chaula ambaye ni baba mzazi wa Shadrack amezungumza na Mwananchi iliyotaka kujua nini kinaendelea juu ya mwanawe huku akisema bado ana maumivu makali na tumbo joto la namna ya kupata Sh3 milioni ili mwanawe arejeshwe akiwa hai au mfu.

“Nakumbuka ilikuwa juzi (Agosti 30, 2024) majira ya jioni nilipigiwa simu nikahojiwa, wewe ni baba wa Shadrack? nikajibu ndio, nikaelezwa mwanao tunaye ukitaka tumuachie tuma Sh3 milioni tutamuachia,” amesema Chaula.

Amesema baada ya mazungumzo na mtu huyo mwenye sauti ya kiume, alimua kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Rungwe Juu ya kile alichoelezwa na mtu huyo ikiwamo kuwasilisha namba hiyo iliyompigia kwa ajili ya uchunguzi kubaini mwanawe yuko wapi ili moyo wake utulie.

“Bado kama familia tuko matumbo joto, hatuli tukashiba, hatuogi tukatakata, tumekaa vikao ambavyo hatupati majibu, tumetafuta kila kona bila mafanikio sasa tupo njia panda tunangoja msaada wa Serikali yetu sikivu,” amesema huku akiwa na kigugumizi cha uchungu.

Baba huyo ameliomba Jeshi la Polisi kuanza upelelezi wa kiintelenjia kufuatilia namba hiyo iliyotumika kupiga kutaka fedha kwa kuwa  wanaweza wakafanikiwa kumpata kijana wake kipenzi.

Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga juu ya taarifa hiyo ya Chaula ya kutakiwa kutoa Sh3 milioni, amesema hajapata taarifa hizo kwa kuwa yuko kwenye mbio za Mwenge akisema analifuatilia.

“Nitafuatilia, nilikuwa kwenye mbio za Mwenge, nipe muda nifanye mawasiliano kwanza,” amesema Kamanda Kuzaga.

Katika mazungumzo baina ya Mwananchi na Chaula, amedai kwa sasa afya yake imeteteleka na mapigo yake ya moyo yapo juu na hajui hatima ya maisha yake kama ataendelea kuwepo duniani kwa kuwa ana maumivu makali.

“Nilienda kutapa vipimo wataalamu wa afya wamenishauri kupunguza mawazo, lakini ndugu mwandishi nawezaje kuyapunguza,  Shadrack alikuwa msaada mkubwa sana kwangu katika mahitaji mbalimbali sasa ni mwezi simuoni nitaishije,” amehoji.

Agosti 7, 2024, Chaula alipozungumza na Mwananchi alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la mwanawe ‘kutekwa’ ili aweze kupatikana.

“Naomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mwanangu apatikane akiwa hai au amekufa maana kutekwa ni sawa na tukio la kuchinjwa kwa mtu,” alisema.

Baba huyo alisema mwanawe mbali na kuwa msanii wa uchoraji, alikuwa akijihusisha na biashara ya duka na maeneo mawili ya kuoshea magari katika Kijiji cha Ntokela huku akishilikiana vyema na vijana wenzake.

Awali, Julai 4, 2024 kijana huyo mwenye miaka 24 alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili baada ya kukiri kosa la kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia, alikutwa na kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.

Hata hivyo, Agosti 2, 2024 katika mitandao ya kijamii kulikuwa na taarifa zinazoeleza Shadrack katekwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari nyeusi kisha kuondoka naye na jitihada za kumtafuta zilikuwa zikiendelea kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Related Posts