Dar es Salaam. Miongo sita iliyopita siku kama ya leo, Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) lilizaliwa baada ya kukamilika mchakato wa kuunganishwa kati ya lile la Zanzibar na Tanganyika.
Jeshi la Zanzibar wakati huo liliitwa la Ukombozi, huku Tanganyika likiitwa Military Force na muungano huo uliunda jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, tangu Septemba 1, 1964.
Kama utahusianisha miaka ya jeshi hilo na umri wa binadamu, kwa miongo sita ni mzee aliyefikia umri wa kustaafu kwa lazima katika utumishi wa umma.
Lakini, umri huo kwa JWTZ ni tafsiri halisi inayoakisi kuzaliwa, kukua, kukomaa na sio kuzeeka kama ilivyo kwa binadamu.
Katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ, maofisa wa jeshi hilo, viongozi na wananchi wamefurika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kushuhudia shamrashamra hizo.
Mbali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakuu wa wilaya zote za Dar es Salaam, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amehudhuria sherehe hizo.
Wengine ni Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Abdulla alifuatiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyefika katika uwanja huo saa 3:19 asubuhi.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda ndiye aliyefuatia, kisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Rais Samia Suluhu Hassan amewasili katika viunga hivyo saa 3:57 asubuhi na kuzunguka uwanja wote akiwa kwenye gari maalumu kusalimia waliohudhuria.
Baada ya kuzunguka mkuu huyo wa nchi aliyekuwa amevalia gwanda la JWTZ, mizinga 21 isiyo na madhara ilipigwa ikisindikizwa na wimbo wa Taifa na beti mbili za wimbo wa Afrika Mashariki.
Kisha, Rais Samia alikwenda kukagua gwaride katika vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na wimbo wa Taifa ulipigwa tena.
Wimbo huo ulifuatiwa na gwaride la vikosi mbalimbali vya JWTZ na lililoonekana kuwavutia wengi zaidi ni lile la wanamaji kutokana na mavazi yake meupe.
Kama ungekuwa nje ya uwanja huo, ungedhani ni kelele za wanaoshangilia mchezo wa mpira wa miguu, lakini shangwe hizo, ziliakisi furaha ya wahudhuriaji juu ya mwendo na matendo sambamba yaliyofanywa na wanagwaride.
Mistari ya vikosi vya ulinzi na usalama hivyo, ilipangwa mithili ya iliyonyooshwa kwa rula na haikuwa hivyo, kwa JWTZ pekee, hata mgambo walikuwa vema.
Nakosa mnyama rahisi wa kumfananisha ukubwa sawia na mbwa walioshuhudiwa na kikosi cha mbwa cha JWTZ, ni wakubwa mithili ya simba jike aliyezaa mara kadhaa.
Gwaride lilipopita mbele ya jukwaa kuu, maaskari waliovalia kijeshi walipiga saluti akiwemo Amri Jeshi Mkuu huyo, Rais Samia.