Dk Ndugulile afunguka hatima ya ubunge wake Kigamboni

Dar es Salaam. Mteule wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile amefunguka na kusema Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam haliko wazi kwa sasa.

Maswali mengi yanayoulizwa ni kuhusu ukomo wa nafasi ya ubunge kwa Dk Ndugulile, ambaye ni Mbunge wa Kigamboni, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk Ndugulile alitoa kauli hiyo usiku wa Agosti 31, 2024 ikiwa ni siku tano kupita tangu aliposhinda nafasi hiyo iliyogombewa na wawakilishi kutoka nchi tano za ikiwamo Tanzania, Niger, Senegal, Rwanda na Ivory Coast.  

Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Dk Ndugulile aliweka wazi kuhusu nafasi yake ya sasa na kwamba atajikita rasmi katika majukumu yake ifikapo Februari 2025.

Alisema kwa sasa yeye bado ni mbunge halali wa jimbo la Kigamboni, mpaka itakapotangazwa kwamba jimbo lipo wazi na kwamba, utaratibu utamtaka ajiuzulu pale atakapothibitishwa kuwa ni mkurugenzi rasmi.

“Bado nitaendelea na majukumu yangu mengine ya kawaida mpaka hapo Februari mwakani, kwa wale wanaosema kwamba jimbo la Kigamboni lipo wazi jibu ni hapana, bado mbunge anaendelea kutimiza wajibu wake kama  kawaida mpaka pale nitakapokuwa nimethibitishwa mwakani nafasi ya ubunge itakuwa wazi,” alisema Dk Ndugulile.

Kwa utaratibu wa WHO ulivyo, Dk Ndugulile ambaye amechukua nafasi ya Dk Matshidiso Moeti kutoka Botswana, katika kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika kilichofanyika Brazzaville DRC, jina lake litawasilishwa kwa uteuzi katika kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji ya WHO, ambacho kitafanyika Februari 2025, Geneva, Uswisi.

Pamoja na hayo, Dk Ndugulile amesema kuteuliwa kwake kuwa msimamizi mkuu wa kanda yenye nchi 47, amepokea kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, huku akiishukuru Serikali ya Tanzania kwa kulipendekeza jina lake.

“Majukumu yangu nitaanza kutekeleza kuanzia Februari mwakani baada ya kuchaguliwa na baadaye kikao cha Bodi ya Utendaji ya WHO kunipitisha kitakachofanyika mwakani,” amesema.

Dk Ndugulile ametaja mikakati yake akisema uongozi wake unakwenda kuleta mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji huduma za afya Afrika.

“Hatua tulizofikia kama bara na hasa katika malengo endelevu ya milenia bado tuko nyuma kidogo, tumeona sisi au mimi kama mgombea tunahitaji kwenda kuongeza nguvu mpya ili nchi za bara la Afrika tuhakikishe tunafikia yale malengo.

“Bara letu bado lina changamoto asilimia 70 ya vifo vyote kinamama vinatoka kwetu, asilimia 56 vifo vya watoto duniani, udumavu asilimia 30 Afrika bado tuna changamoto nyingi na mimi uzoefu wangu kama mtaalamu nimefanya masuala ya afya ndani na nje ya nchi, Waziri katika wizara mbalimbali, uzoefu wa kisiasa kama mbunge hili litakwenda kuwa na mwitikio mzuri katika bara la Afrika,” amesema.

Hata hivyo, suala kuhusu ukomo wake liliwahi kuzungumzwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, January Makamba, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi huo Mei 2024 akisema: “Kigamboni watakukosa, lakini Afrika watapata jembe. Dk Ndugulile ametumika hapa nchini na sasa anakwenda kutumikia nafasi nyingine iwapo kura zitaamua.”

Related Posts