JKU, Chipukizi na leo tena Zenji

PAZIA la msimu mpya wa mashindano kwa visiwani Zanzibar, linafunguliwa jioni ya leo kwa timu za JKU na Chipukizi kukutana katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex mjini Unguja na kukumbushia kisanga cha pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho lililovunjika.

JKU ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) na Chipukizi waliobeba Kombe la Shirikisho msimu uliopita, wanakutana tena baada ya pambano lao la fainali hizo za Kombe la ZFF, lililopigwa visiwani Pemba lilivunjika kabla ya muda kutokana na maafande wa JKU kulianzisha kwa kumpiga mwamuzi.

Pambano hilo lilimaliza dakika 90 matokeo yakiwa 1-1 na ziliongezwa dakika 30 na kwenye dakika ya 103 JKU ilipata bao lililokataliwa na mwamuzi Mohammed Amour Ngwali kwa madai ya mfungaji kuotea na kumvamia, jambo lililovunja pambano hilo na kusababisha timu hiyo kuadhibiwa na ZFF.

JKU ililimwa fauini ya Sh 2 milioni, huku mwamuzi akitozwa Sh 500,00 0 na kusimamishwa kwa miezi mitatu kwa kosa alilofanya, mbali na Chipukizi kulimwa Sh 1 Milioni kutokana na mashabiki wake kurusha chupa uwanjani kupinga kilichotokea, huku klabu ikipewa ushindi wa mezani na tiketi ya mechi za CAF.

Hata hivyo, Chipukizi haikushiriki kutokana na madai ya kuwa na hali mbaya kiuchumi na nafasi yake ilichukuliwa na Uhamiaji iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa raundi ya kwanza na Al Ahly Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 5-1, huku JKU iking’olewa na Pyramids ya Misri Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 9-1. Tripoli itacheza sasa na Simba kwenye mechi za raundi ya pili kuwania tiketi ya makundi kwa msimu huu wa michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Achana na kisanga hicho cha msimu uliopita, leo timu hizo mbili zinakutana tena katika pambano la Ngao ya Jamii litakalopigwa kuanzia saa 10:00 jioni na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga alisema mapema jana kuwa maandalizi ya mchezo yamekamilika.

Kuchezwa kwa mechi hiyo leo ni ufunguzi rasmi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar itakayoanza wiki ijayo ikishirikisha jumla ya klabu 16, zikiwamo nne mpya zilizopanda daraja ambazo ni Muembe Makumbi City, Inter Zanzibar za Unguja pamoja na Junguni FC na Tekeleza za Pemba.

Timu hizo nne mpya zimechukua nafasi ya timu za Kundemba, Ngome, Jamhuri na Maendeleo zilizoshuka kutoka Ligi Kuu msimu uliopita ulioshuhudiwa JKU ikiivua ubingwa KMKM kwa kuvuna pointi 66 kwa mechi 30.

Related Posts