Songwe. Wakazi wa miji ya Itumba na Isongole wilayani Ileje Mkoa wa Songwe wameiomba Serikali kuharakisha ujezi wa mradi wa maji unaojengwa kwa gharama ya Sh 4.9 bilioni ili kutatua changamoto ya huduma hiyo.
Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wananchi takribani 20,000 wa eneo hilo.
Wananchi wametoa maombi hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo jana Aprili 30,2024 wakati akikagua ujenzi wa mradi unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(Ruwasa) kwa nguvu ya wananchi (Force Account).
Mkazi wa Kijiji cha Itumba, Edward Chibona amesema kinamama wanatumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za kiuchumi.
Mkazi mwingine, Sekela Shibanda ameiomba Serikali iwasaidie kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kuwanusuru kinamama kuhangaika kupata maji salama.
Meneja wa Ruwasa wilayani Ilaje, Mhandisi Endrew Tesha amesema mradi huo umefikia asilimia 85 hivyo wanahitaji Sh350 milioni kutoka ndani ili kutekeleza mradi huo.
“Kukamilika kwa mradi huo kutaondoa adha ya uhaba wa maji kwa wananchi 20,000 wa vijiji vya Itumba, Isongole, Ilulu na Izuba; na wamefanikiwa kujenga tenki lenye ujazo wa lita laki tano pamoja na chujio la kuchuja maji,” amesema Mhandisi Tesha.
Mkuu wa wilaya hiyo, Farida Mgomi amesema mradi huo tangu umeanza kutekelezwa na Ruwasa umetekelezwa kwa kasi, hivyo ukikamilika wananchi wataondokana na majisafi na salama.
Mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo amesema kutokana na mahitaji ya maji kwa wananchi kuwa makubwa, atawasiliana na waziri wa maji asaidie kuweka msukumo wa kutoa Sh350 milioni ili wananchi waanze kunufaika na mradi huo.