Dar es Salaam. Wanataaluma 16 wa Tanzania wanatarajia kuanza safari yao ya kimasomo nchini Japan.
Wanataaluma hao watasoma shahada za uzamili na kupata uzoefu kwa vitendo kupitia mafunzo ya kazi katika kampuni za kijapani.
Wanufaika hao chini ya Mpango wa Elimu ya Biashara kwa Vijana wa Afrika (ABE Initiative-African Business Education Initiative for Youth), huku ukiwezeshwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica).
Mpango huo unawapa vijana wa kiume na wa kike wa Kiafrika fursa ya kusoma katika vyuo vikuu vya Japani na kupata uzoefu wa vitendo kupitia mafunzo ya kazi katika kampuni za nchini humo.
Katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwakilishi Mkuu wa Jica, Ara Hitoshi amewataka washiriki hao kuyatumia maarifa watakayoyapa kwa ajili ya kujenga maendeleo ya Tanzania watakaporejea.
“ABE Initiative ni uthibitisho wa ushirikiano imara na unaokua kati ya Japan na Tanzania. Nawaomba nyote mshiriki kikamilifu katika masomo na mafunzo ya kazi na mtakaporudi tumieni maarifa na ujuzi wenu katika kuchangia maendeleo ya Tanzania, mustakabali wa ushirikiano wetu uko mikononi mwa wataalamu wenye uwezo kama mtakaoupata nyinyi,” amesema Hitoshi.
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa pia alizungumza na wanazuoni waliomaliza muda wao na kuwataka kujikita katika utamaduni na mfumo wa elimu wa Japan, huku akisisitiza thamani ya kuelewa tofauti za kitamaduni kama sehemu muhimu ya safari yao ya kielimu.
“Unapoingia katika sura hii mpya, nakuhimiza ujiunge na shughuli mbalimbali ili kujifunza zaidi kuhusu Japan na kupanua uelewa wako wa nchi yetu na utamaduni wake. Ingawa unaweza kukutana na changamoto kutokana na tofauti za kitamaduni, zichukulie kama fursa za kujifunza. Kuwa muwazi, akili na kuthamini uzoefu,” amesema Misawa.
Miongoni mwa walionufaika mwaka 2024 ni Rita Lema kutoka Wizara ya Fedha ambaye alielezea furaha yake kuhusu fursa ya kusoma nchini Japan, huku akiweka wazi malengo yake ya kujifunza juu ya uchumi wa kidijitali na uwezekano wa kutekeleza zana za sarafu mtandao.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo na mnufaika wa mpango wa ABE wa mwaka 2019, Beno Kiwale alielezea mafanikio yake na kuonyesha faida za mpango huo.
“Mpango wa ABE ulinipa fursa ya kipekee sio tu kuongeza ujuzi wangu wa kitaaluma lakini pia kupata maarifa ya vitendo kupitia mafunzo ya kazi. Uzoefu huu wa vitendo ulikuwa muhimu katika kuvutia uwekezaji wa Japan kuja Tanzania na kunufaisha tasnia yetu ya ndani,” amesema Kiwale.