BEKI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga FC Lupopo ya DR Congo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefungukia fursa iliyopata timu anayoichezea kwa sasa kukutana na Bravos do Maquis raundi ya pili za Kombe la Shirikisho Afrika, huku akikiri haitakuwa mechi rahisi kutokana na ubora wa Waangola.
Bravos ilipenya hatua hiyo baada ya kuvuka raundi ya kwanza kwa kuing’oa Coastal Union ya Tanzania kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0, huku kina Ninja Lupopo wakipangwa kuanzia raundi hiyo ya pili kama ilivyo kwa Simba itakayovaana na Al Ahli Tripoli iliyoing’oa Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1.
Ninja alisema ni Bravos ni miongoni mwa timu bora inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola, hivyo wamejiandaa kama timu kupambana kuhakikisha inapata ushindi.
“Ni timu ambayo kocha ameelekeza ubora na udhaifu wao na tumeanza kufanyia kazi mazoezini kama mlinzi nina kazi ya ziada kuisaidia timu yangu na naamini malengo ya kufika mbali yatatimia na kwa upande wangu itakuwa jambo zuri,” alisema Ninja nyota wa zamani wa Taifa Jang’ombe, Yanga, Dodoma Jiji aliyewahi kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na Marekani.
Lupopo itaanzia ugenini Sepemba 13 kwenye Uwanja wa Estadio Nacional da Tindavala kabla ya kuvaana Congo Septemba 20 Uwanja wa Stade des Martyrs.
Kabla ya kutua FC Lupopo, Ninja msimu uliopita alikuwa akikipiga klabu ya FC Lubumbashi pia ya DR Congo.