Arusha. Wataalamu wa sayansi, teknolojia na mazingira wameanza utafiti wa kuimarisha upatikanaji wa mahitaji muhimu ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu Tanzania imeongezeka kwa asilimia 37, kutoka watu milioni 44.92 mwaka 2012 hadi kufikia milioni 61.74.
Shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria kuwa idadi ya watu inaweza kufikia zaidi ya milioni 120 ifikapo mwaka 2050.
Kutokana na ongezeko hilo, wataalamu wanachukua tahadhari kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kama chakula, maji, usalama wa mazingira na mawasiliano.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Septemba Mosi, 2024 katika mahafali ya 10 ya wahitimu 92 wa shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na mtafiti Denis Mwalongo.
Amesema lengo la utafiti huo ni kuisaidia Serikali kukabiliana na ongezeko la watu kwa kugeuza changamoto kuwa fursa.
“Tunaona viashiria vya tatizo na tumeanza utafiti mapema ili kutafuta njia bora ya kukabiliana na ongezeko la watu,” amesema Mwalongo.
Hata hivyo, amesema changamoto iliyopo sasa ni namna ya kupata mahitaji muhimu kama chakula, huku ardhi ikiwa haiongezeki.
Hata hivyo, amesema watafiti hao wanatafuta njia nzuri za kulinda mazingira na bionuwai zilizopo ili kuhakikisha ustawi wa binadamu na viumbe wengine unaendelea kuimarika.
“Utafiti pia utazingatia upatikanaji endelevu wa maji safi na salama, miji inavyokua vyanzo vya maji navyo vinapungua jambo linaloweza kuhatarisha maisha ya watu,” amesema.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula amesema asilimia 85 ya wanafunzi waliohitimu wamepata udhamini kutokana na tafiti zao za kutatua changamoto za kijamii. Na amewasisitiza wanafunzi na hasa vijana, umuhimu wa kutumia teknolojia za akili bandia na mashine za kuhisi ili kuchangamkia fursa na kuleta mageuzi katika sekta ya kiuchumi na huduma.