Vigogo KenGold wameamua | Mwanaspoti

WAKATI benchi la ufundi Ken Gold likiahidi kusuka kikosi upya, uongozi wa timu hiyo nao umekoleza moto kwa mastaa ukiahidi dau nono kwa matokeo ya ushindi kuanzia mchezo ujao dhidi ya Fountain Gate.

Ken Gold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza haijaanza vyema msimu, baada ya kupoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Singida Black Stars kwa kichapo cha 3-1 nyumbani.

Timu hiyo ambayo inaendelea na mazoezi huko Igawilo jijini Mbeya inatarajia kushuka tena uwanjani Septemba 11 kuwafuata Fountain Gate mkoani Manyara katika muendelezo wa ligi hiyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema anaendelea kutengeneza kikosi upya kutengeneza muunganiko na kwamba hadi mchezo ujao nyota wake watakuwa fiti na kuipa matokeo mazuri.

Alisema mechi ya kwanza haikuwa nzuri kwao, lakini vijana hawakuwa wanyonge kutokana na kiwango walichoonesha licha ya ugeni walionao baadhi ya wachezaji.

“Tunaendelea na mazoezi kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kiushindani, kimsingi hatujapoteza muelekeo na vijana wana ari na morali, tunaamini mechi ijayo furaha itaanza” alisema Elias.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha alisema kwa sasa uongozi umetenga dau nono kwa wachezaji ambapo kila mchezo wa ushindi watakabidhiwa mzigo wa maana.

“Tayari taarifa wanazo kambini, hili tumelifanya kwa ajili ya kuongeza motisha na morali kuhakikisha tunapata ushindi kila mchezo, hatujatangaza wazi kiwango kwakuwa ni siri yetu na wao”  alisema Katibu huyo.

Related Posts