Dar es Salaam. Wakati maandalizi ya chaguzi zijazo yakiendelea nchini, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu ameonyesha hofu kwa yanayoendelea kama yatachagiza kupata viongozi bora.
Kiongozi huyo wa kiroho amewataka Watanzania katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 kutafuta mtu atakayewasaidia na kutanguliza mbele utu na ubinadamu.
Askofu Dallu amesema hayo leo Jumapili, Septemba mosi, 2024 katika Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya miaka 25 ya upadri wa Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa na miaka 50 ya upadri wa Askofu mstaafu wa jimbo hilo, Bruno Ngonyani.
Misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Pisa imefanyikia Uwanja wa Ilulu, Lindi mjini na kuhudhuriwa na maaskofu, mapadri, watawa wa kiume na kike, waumini, wanasiasa na viongozi wa Serikali akiwemo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi (DC), Shaibu Ndemanga aliyemwakilisha mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack.
Mbali na DC huyo, wengine ni wabunge, Nape Nnauye (Mtama) na Hamida Abdallah wa Lindi, Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Profesa Adelardus Kilangi na Ngusa Simike, aliyekuwa Katibu wa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.
Katika mahubiri yake, Askofu Dallu amesema kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, kuna viongozi watajitokeza kutupiana lawama kwa kuhisi mwenzake ndiye chanzo cha kutofanyika kwa yale yaliyotarajiwa na wananchi.
Askofu Dallu amewataka wananchi wanapojitokeza watu wema kuomba kura, waache kuwaomba chochote kwa kutumia kauli “Unatuachaje?” kisha baadaye wanaanze kulia kwa Serikali kwa kuchagua watu wasio sahihi.
“Tena siku hizi wanahalalilisha kabisa, wewe kula hela halafu kura mpe mwingine, huo ni uongo maana watu mnaogopa kama washirikina wanaogopa kurogwa, ukila cha mtu lazima kura umpe. Umepanda dhambi, matunda yake lazima uyapate,” amesema Askofu Dallu.
Amewataka watafute mtu atakayewasaidia na si kusema hakuna mtu, kwani watu kwa sasa wamekusanya fedha nyingi kwa ajili ya kuwapatia wananchi kuelekea kwenye uchaguzi.
Kuhusu ubabe wa viongozi wanaopewa madaraka, kiongozi huyo amesema kuna kipindi ambacho waliita cha mageuzi na mapinduzi ya Ufaransa ambapo viongozi wa taasisi za kidini na utawala walikuwa wanajitambulisha katika jamii kuwa wao ndiyo taasisi.
“Viongozi wa taasisi za dini na za utawala wa kiserikali walikuwa wakijitambulisha wao ni kanisa au Serikali, hivyo ukiniona mimi ujue umeliona kanisa na wale wa kiutawala walisema Serikali, hivyo viongozi wa kijamii na wa kidini sio viongozi wazuri wa taasisi zao,” amesema Askofu Dallu.
Amesema chochote walichoamua na kufanya kwa niaba ya taasisi zao kiliharibu mategemeo ya taasisi wanazozisimamia na watu wanaowaongoza.
Kutokana na matendo hayo, viongozi hao wametengeneza chuki kati ya jamii na taasisi wanazozisimamia ambapo uongozi wa taasisi husika wanakuwa wamewaamini kiasi cha kuona bila hao taasisi zao haziwezi kwenda na kukwama kabisa.
Askofu Dallu amesema wasione haya kwa taasisi husika kukanusha kwa yale yanayoendelea ili kuacha kuwasifu, kwani wanaweza kufanya hivyo watakapokufa.
“Atatokea mtu ameharibu hali ya hewa huko ambapo walikuwa wanajitambulisha wao kama ndiyo taasisi wanazozisimamia za kidini na kiutawala wakidai ukiniona mimi umeliona kanisa au Serikali, hivyo wakiharibu taasisi husika zinatakiwa kuomba radhi hata kwa matukio ya nyuma,” amesema Askofu Dallu.
Amesema watu wa namna hiyo hawakosekani, ni sehemu ya maisha hivyo lazima kupangana vizuri ili iwe kwa nia njema, kwani wapo ambao wanaweza kutumia mamlaka vibaya na kuharibu hata kazi za watu wa usalama kwa kutoa amri kwa kupigania mradi alionao.
“Anaweza kuamrisha kwa sababu ana mradi nendeni mkapige kile kijiji chote wanatupinga, unamuharibia hata mtu wa ulinzi na usalama, unatumia mamlaka vibaya na anaumia, anaendaje kwa sababu huo si utaratibu anafanya wewe ni bosi wake,” amesema.
“Hauwakilishi kilichokuwepo, unawakilisha udhaifu wako na hautaki kuungama,” amesema.
Pia, amesema kipindi cha uchaguzi wapo viongozi wana uhakika wa ushindi wa asilimia 90, lakini bado watakuwa wanazitaka na zile za asilimia 10 za mtu mwingine aziweke kwake, hivyo wanazidi kujiongezea dhambi.
Naye Askofu Ngonyani katika maelezo yake amewashukuru kwa zawadi na kumwomba Mungu kuwajaalia wote: “Na Askofu Pisa, pamoja na wote ili kuchangia maendeleo ya jimbo letu. Napata muda mwingi wa kustarehe, kusali, kutembea hapa na pale nitaendelea kukuombea (Askofu Pisa).”
Askofu Pisa amesema mwaka wa Jubilei ni wa kuomba msamaha na anaomba msamaha kwa Mungu pale aliposhindwa kutimiza majukumu yake kama padri.
“Jukumu la padri ni kumkiri na kujipoteza katika Kristu, ni kuendelea kumkiri na kujipoteza zaidi huku wakiendelea kuwaelekeza watu kwa kuwapeleka kwa Yesu Kristu,” amesema Askofu Pisa.
Pia ametoa wito kwa waumini wa jimbo la Lindi kuendelea kutoa michango waliyojiwekea kwa miaka mitano, kwani watakuwa wamejenga kanisa litakaloingiza waumini 2,000 ambalo litagharimu Sh6.6 bilioni
DC Ndemanga amesema changamoto zilizoelezwa na Askofu Dallu watazifanyia kazi na ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi bora ambao hawataweka rushwa mbele.
“Tumesikia changamoto alizozieleza Askofu, tumepokea ushauri na tutakwenda kufanyia kazi.
“Niwaombe wana Lindi twendeni tukajiorodheshe kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa, yapo ambayo tumeshauri hapa hatuwezi kuyaondoa kama hatujajiandikisha ili kuchagua viongozi bora ambao hawataweka rushwa mbele.”
Amesema mapambano ya rushwa yafanyike kwa watu wote ambapo watu wakiwa nje ya nyumba za ibada ni wa Serikali, hivyo wanapoingia kanisani na msikitini wawaambie hawataki rushwa.
Pia, amesema wameshamaliza kufanya thatmini ya matengenezo ya ujenzi wa barabara mpya ya Mtwara hadi Masasi, kwani imekuwa kero na Serikali inakwenda kujenga upya barabara hiyo pamoja na ile ya Lindi hadi Dar es Salaam.
Kuhusu uharibifu wa barabara ya Ruvuma kwenda Mtwara, amesema baada ya miaka kadhaa wataacha kuona malori yanayobeba makaa ya mawe, kwani Serikali inaendelea na taratibu zake za ujenzi wa reli.