IMEELEZWA kuwa, Namungo FC ipoa katika mazungumza na kocha mkuu wa timu ya soka ya Wanawake ya Simba Queens, Juma Mgunda ili kwenda kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera anayetarajiwa kupigwa panga baada ya kuanza vibaya mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu.
Namungo ilianza msimu kwa kufungwa mabao 2-1 na Tabora United kisha kulala tena 2-0 mbele ya Fountain Gate kitu kilichoondoka na Mtendaji Mkuu, Omar Kaya aliyeamua kujiwajibisha mwenyewe kwa kutanga kujiuzulu saa chache baada ya kipigo cha pili na uongozi wa klabu hiyo kuridhia kuondoka kwake.
Chanzo kutoka ndani ya Namungo kinasema kuwa, mmoja wa vigogo wa ngazi ya juu wa timu hiyo, ndiye aliyepiga simu kwa Mgunda kumhitaji kuja kuinoa timu.
Chanzo hicho kinasema kuwa, tayari viongozi walishamalizana na Zahera na kilichobaki ni kutangazwa tu juu ya kuondoka klabuni hapo.
“Huyo kigogo ndiye alikuwa na kikao na Mgunda, hivyo lolote linaweza likatokea, ambapo dili lake likitiki msaidizi wake anaweza akawa Ngawina Ngawina aliyepo Coastal Union,” kilisema chanzo hicho.
Ilitajwa sababu ya kuhitaji huduma ya Mgunda ni uzoefu alionao, kuanzia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na pia kuisaidia Simba kipindi cha mpito baada ya kuachana na kocha Zoran Maki wakati huo akitokea Coastal, klabu aliyowahi kuichezea na kuinoa kwa nyakati tofauti.
Katibu wa timu ya Namungo, Ally Seleman alipotafutwa ili kuthibitisha taarifa hizo za Mgunda kutakiwa na klabu hiyo alisema hizo ni tetesi, lakini hadi kufikia leo Jumatatu) huenda kila kitu kikaa sawa.
“Hizo ni tetesi ambazo siwezi kusema ndio ama hapana, tusubiri muda utaongea nadhani kuanzia kesho (leo) Jumatatu ukweli utajulikana,” alisema Seleman.
Ukiachana na Namungo kumhitaji Mgunda, pia taarifa nyingine zinasema matajiri wa Chamazi, Azam FC imekuwa ikimpigia hesabu kocha huyo ili kuiongoza kipiti cha mpito kwani wamebaki kutangaza tu juu ya hatma ya kocha Youssouf Dabo anayedaiwa amepigwa chini kutokana na timu kung’oka mapema Ligi ya Mabingwa Afrika ikitolewa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1.