WAKATI wadau mashabiki wa soka wakisubiri tukio la Mbeya City Day, uongozi wa timu hiyo umesema maandalizi yanaenda vyema na wamejipanga kuwapa raha wakazi wote wa jiji hilo.
Awali tukio hilo lilikuwa lifanyike Agosti 17 mwaka huu, kisha kusogezwa hadi Agosti 31, lakini sasa ni rasmi litafanyika Septemba 7 ambayo ni Jumamosi ya wiki hii, huku ikichagizwa na wasanii na wachekeshaji mbalimbali.
Mbeya City inayojiandaa na Championship msimu wa 2024/25, inaendelea na kambi yake huko Mwakaleli mji mdogo wa Tukuyu, inatarajia kurejea jijini hapa kati ya kesho au keshokutwa.
Hadi sasa timu hiyo iliyodumu miaka 10 mfululizo Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja misimu miwili nyuma, haijatangaza kikosi chake wala benchi la ufundi na jezi huku matukio yote hayo yakitarajiwa kufanyika kwa wakati mmoja Jumamosi katika Mbeya City Day.
Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema hadi sasa maandalizi yamefikia patamu, ambapo katika tamasha hilo litaambatana na utambulisho wa wachezaji na kuzindua jezi.
Alisema katika tukio hilo la kihistoria, wamealika timu ya Ligi Kuu nchini Zambia, Real Nakonde kwa ajili ya mchezo wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
“Tutakuwa na watu mbalimbali kusherehesha tamasha hilo, tutatambulisha kikosi, benchi la ufundi na kuzindua rasmi jezi za msimu ujao, kwa ujumla maandalizi yanaendelea vyema,” alisema Nnunduma.
Mmoja wa wadau wa soka jijini Mbeya, Fikiri Masai alisema msimu ujao wanayo matumaini na timu hiyo kurejea Ligi Kuu kutokana na maandalizi waliyonayo na mipango ya nje ya uwanja kwa uongozi.
“Sisi tunaifuatilia sana timu yetu, usajili uliofanyika ni mkubwa na wa kimkakati, uongozi unajitahidi na umetuweka karibu tofauti na misimu iliyopita, tunaamini tutarejea Ligi Kuu,” alisema Masai.