Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya soka ya Simba, Muharami Sultani(40) na wenzake, limepelekwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akishirikiana na Frank Rimoy ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Septemba 2, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Sultani na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka nane, yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.
Mwanga alitoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
“Kwa kuwa jalada hili limepelekwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amedai Grace.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hadi Septemba 16, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.
Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif, Said Matwiko mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu kama Mbonde, mkazi wa Kisemvule ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami.
Wengine ni John John maarufu kama Chipanda, mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manane, likiwemo la kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini hydrochloride.
Shtaka la pili inadaiwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 27.10.
Vilevile, Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 7.79.
Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa Aprili 15, 2021 katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies Ltd, huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Katika shtaka la nane inadaiwa Aprili 20, 2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies Ltd, akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.