Tarura yataja vipaumbele ujenzi wa barabara, matumizi ya teknolojia mpya

Dar es Salaam. Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) umetaja vipaumbele vinne katika utendaji wao, ikiwemo kutumia teknolojia zinazohusisha kutumia malighafi zinazopatikana eneo la kazi kupata ufanisi wa gharama za ujenzi.

Kipaumbele kingine ni kutunza barabara zilizopo katika hali nzuri na wastani kubaki kwenye hali hiyo, ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika na kuondoa vikwazo kwenye mitandao ya barabara ili zipitike misimu yote.

Pia kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa changarawe na changarawe kuwa lami, kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi kimataifa na kimataifa.

Hali hiyo inachochewa na ufinyu wa bajeti  ya Tarura ambayo kwa mahitaji yao halisi kwa mwaka ni Sh1.3 trilioni, lakini wamepatiwa Sh850 bilioni, fedha ambazo hazitoshi  kutokana na ongezeko la idadi ya watu na mahitaji kubadilika, licha ya kuongezeka mara tatu kutoka Sh275 bilioni.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Septemba 2, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seff  katika mkutano wa waandishi na wahariri wa vyombo vya habari  uliandaliwa na Msajili wa Hazina, mamlaka hiyo kuelezea miaka mitatu ya mafanikio  ya usimamizi wa mtandao wa barabara za wilaya kuanzia 2021/2022 hadi 2023 / 2024.

“Tathmini iliyofanyika mwaka 2022/2023 ilibaini Sh1.35 trilioni zinahitajika kuanzia 2023/2024, ili asilimia 85 ya mtandao wa barabara za wilaya ipitike misimu yote, sasa Tarura inapata wastani wa Sh850 bilioni kwa mwaka,” amesema.

Mtendaji huyo amesema ili kupata ufanisi katika ujenzi kulingana na fedha zilizopo, wanatumia teknolojia ya kuboresha udongo kabla ya kuweka lami (Ecoroads).

Hadi sasa amesema kwa kutumia teknolojia hiyo, jiji la Dodoma tayari kilomita moja imejengwa na Wilaya ya Chamwino kilomita 6.95 na zote zimekamilika.

“Wilaya ya Rufiji zimejengwa kilomita 32 kwa kutumia teknolojia ya kokoto (Ecozyme) na Wilaya ya Itilima kilomita 5.2, tunatuma malighafi kama mawe ambayo hupunguza asilimia zaidi ya 50 ya gharama na tayari tumejenga madaraja 275 na kilomita 225 za barabara kwa kutumia mawe,” amesema.

Akizungumzia ujenzi wa barabara nchini, Seff amesema mtandao wa barabara za wilaya umeongezeka kutoka kilomita 108,946.19 hadi kilomita 144,429.77 kufikia Juni 2024.

Kwa upande wa changarawe, Seff amesema hadi kufikia Juni, barabara za wilaya zimefikia kilomita 42,059.17 na lami kilomita 3,337.66.

Akizungumzia Mkoa wa Dar es Salaam, amemsema nyumba nyingi zimejengwa katika mkondo wa maji.

Kutokana na hali hiyo, amesema Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP II), unakwenda kuboresha maeneo mengi ya jiji hilo.

“Mradi huu utakuwa ndani ya Halmashauri tano za jiji la Dar es Salaam na utatekelezwa kwa miaka sita, barabara kilomita 250 zitajengwa, mifereji ya kilomita 90, vituo vya mabasi tisa, masoko 18, madampo matatu na wanufaika wa mradi ni wananchi milioni 3.98,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa DMDP II, Nyariri Nanai amesema masoko yatakayoboreshwa ni Tegeta Nyuki, Sinza, Msumi  na masoko matatu ya samaki,jijini Dar es Salaam.

Kwa maeneo ya taka, Nanai amesema maeneo ya kutupa taka yatajengwa Wilaya ya Kigamboni, Ilala na Kinondoni  na pia stendi ya mabasi Tegeta na Kigamboni nazo zikiboreshwa.

Related Posts