Kahawa kuuzwa kwa ‘bajaji’ kukuza soko

Dodoma. Katika kuongeza masoko ya kahawa inayozalishwa nchini, Serikali imebuni na kutengeneza migahawa inayotembea kwa kutumia pikipiki za miguu mitatu kwa ajili ya kuuza kahawa katika maeneo mbalimbali ya umma na kwenye mikusanyiko ya watu.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema leo Jumanne Aprili 30, 2024 wakati wa kujibu swali la msingi la Mbunge wa Vwawa, Japhet Kasunga.

Katika swali lake, Hasunga ametaka kujua mkakati mahsusi wa Serikali wa kutafuta masoko ya kahawa.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema tasnia ya kahawa inatekeleza mkakati wa miaka mitano wa Maendeleo ya Tasnia ya Kahawa (2021–2025).

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Jumanne, Aprili 30, 2024. Picha na Merciful Munuo

Amesema malengo ya mkakati huo ni kuongeza wigo wa masoko, kuongeza mauzo ya kahawa katika soko la ndani kutoka asilimia 7 hadi asilimia 15 ya kahawa yote inayozalishwa nchini.

Silinde amesema ili kutimiza lengo hilo Serikali imeweka mazingira mazuri ya biashara ili kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kuongeza thamani yaliyosababisha ongezeko la viwanda kutoka 21 hadi kufikia viwanda 37 vilivyopo sasa.

“Pia, kuongeza kodi kwa bidhaa za kahawa zinazotoka nje ya nchi kutoka asilimia 25 mpaka 35 ya thamani ya kahawa,” amesema Silinde.

Pia, amesema kuna mkakati wa kubuni na kutengeneza migahawa inayotembea kwa kutumia pikipiki za miguu mitatu zitakazotumika katika uuzaji wa kahawa katika maeneo mbalimbali ya umma na kwenye mikusanyiko ya watu.

Silinde amesema pia kuondoa kodi kwenye vifungashio vya kahawa ambavyo kwa kiasi kikubwa vinapatikana nje ya nchi.

Katika swali la nyongeza mbunge wa viti maalumu, Anatropia Theonest (Chadema) ametaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwawezesha wakulima wa kahawa kupata fedha zao mapema ili ziwasaidie katika kuanda mashamba.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema moja ya mkakati ni kuhakikisha kahawa inauza kwa njia ya mnada ili wakulipa wapate fedha zao kwa wakati na kuwa Serikali itahakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.

Related Posts