Kijiji chapata huduma ya maji miaka 40 baada ya kuanzishwa

Songwe. Wakati Mwenge wa Uhuru ukizindua mradi mkubwa wa maji utakaowanufaisha wananchi zaidi ya 7,000 katika Kijiji vya Chimbuya, Kata ya Ukwile wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe, mkazi wa eneo hilo, Flonsia Mapumba amesema Serikali imenusuru ndoa zao.

Mapumba amesema walikuwa wakitembea umbali mrefu kusaka maji na kutokana na umbali huo, wanawake wengi walikuwa wakiingia kwenye migogoro na waume zao kutokana na kuchelewa kurejea nyumbani.

Mkazi huyo amesema hayo leo Jumatatu Septemba 2, 2024 wakati mradi huo uliogharimu Sh535.7 milioni ukizinduliwa rasmi na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Godfrey Mzava.

“Serikali imenusuru ndoa zetu sisi wanawake kwa kusikia kilio chetu na kutuletea huduma ya maji karibu, tumepata vipigo, masimango na wengine walikuwa wanatishiwa kuachwa na waume zao kisa maji,” amesema Mapumba.

Amesema kwa adha waliyoipitia amewasihi wananchi wenzake wawe walinzi namba moja wa mradi huo ili udumu.

Kijiji hicho ambacho kipo Kata Ukwile, hakijawahi kupata huduma ya maji safi na salama tangu kianzishwa miaka 1980.

Naye Happiness Mgeta, mkazi wa Kijiji cha Chimbuya amesema kabla ya mradi huo, walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata maji maeneo yaliyo na makorongo.

“Hata kwenye hayo makorongo tulikuwa tunapanga foleni kuyachota, unaweza kukaa hata dakika 20 ndiyo unajaza ndoo ya lita 20,” ameeleza Mgeta.

Hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuwajengea mradi huo ambao uko jirani na makazi yao.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(Ruwasa) wilayani Mbozi, Mhandisi Ismail Ismaili amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 17,2023 ukitekelezwa na mkandarasi Saditech Investment Limited  na sasa umekamilika.

Mhandisi Ismail amesema katika mradi huo, tanki lenye ujazo wa lita 250,000 limejengwa ambapo lita 8,740 zinazalishwa kwa saa na wananchi kuchota maji karibu na makazi yao.

“Uunganishaji wa maji majumbani kwa wananchi wa kijiji cha Chimbuya kwa kuwafungia wateja mita za maji ambao hulipia Sh 1,500 kwa unit moja,” amesema Mzava.

Amesema kati ya vituo 11 vya kuchotea maji, vituo vitano vinajiendesha vyenyewe ambapo wananchi hutumia kadi za malipo ya kabla zinazotumia mfumo wa kielektroniki na kulipa Sh40 kwa lita 20 na vituo sita vinaendeshwa na wakala wa jumuiya za watumia maji.

Akizungumza katika uzinduzi huo, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzava amesema mradi huo utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji ambayo awali yalikuwa si safi na salama.

“Kilio cha wananchi wa Chimbuya tangu kuanzishwa miaka ya 1980 ilikuwa ni kupata huduma ya maji karibu, hivyo niwasihi tunzeni miundombinu hii ya maji ili idumu kwa mda mrefu,” amesema Mzava.

Mwenge wa Uhuru wilayani Mbozi umekagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi saba yenye gharama ya Sh 9.7 bilioni.

Related Posts