Marekani imezitaka nchi zote zinazopeleka silaha kwa pande mbili zinazopambana katika vita nchini Sudan kusitisha hatua hiyo.Marekani imeonya kwamba historia inajirudia katika jimbo la Darfur,Magharibi mwa Sudan ambako yaliwahi kushuhudiwa mauaji ya halaiki miaka 20 iliyopita.
Kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan kilikuwa cha faragha na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas -Greenfield aliwaambia waandishi habari baada ya kikao hicho kwamba hali katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur inatisha na historia ya mauaji inajirudia.
Katika mji mkuu wa Darfur,Elfasher ambao ndio mji pekee kwenye jimbo hilo usiodhibitiwa na wanamgambo wa RSF kunashuhudiwa mauaji makubwa.
Thomas-Greenfield amesema kuna ripoti za kuaminika zinazoonesha , wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na jenerali Hamdani Dagalo wamevizingira vijiji vingi magharibi mwa mji mkuu wa El Fasher na wanapanga kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji huo.Na akatowa ujumbe huu kwa RSF
“Wanamgambo wa RSF wanapaswa kusitisha mzingiro na kuondowa wapiganaji wake katika mji wa EL-Fasher na kujizuia kufanya shambulio lolote dhidi ya mji huo.Pande zote katika mgogoro huu zinapaswa kuchukuwa hatua za dharura kuachana na vita.”
Mwanadiplomasia huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametowa tahadhari kwamba ikiwa mji wa El Fasher utashambuliwa litakuwa janga juu ya janga kwasababu watu milioni 2 wanaoishi kwenye mji huo pamoja na wakimbizi 500,000 kutoka maeneo mengine ya Sudan waliokimbilia kwenye mji huo kutafuta hifadhi watakuwa katika hatari kubwa.
Mkuu wa shughuli za kisiasa wa Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo aliwahi kuliambia baraza hilo la usalama mnamo Aprili 19 kwamba vita vya Sudan vilivyodumu mwaka mmoja sasa vimechochewa zaidi na silaha zinazoingizwa nchini humo na mataifa ya kigeni yanayounga mkono pande tofauti katika vita hivyo.Mataifa yanayoingiza silaha sudan yanakwenda kinyume na vikwazo vya Umoja wa Mataifa vinavyolenga kusaidia kumaliza mgogoro huo,na kitendo hicho hakikubaliki.Soma pia: Sudan yautuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu kuwasaidia RSF
Kauli hiyo imeungwa mkono tena katika kikao cha jana na Marekani kupitia balozi wake katika Umoja huo wa mataifa,Linda Thomas Greenfield akisema mataifa yenye nguvu katika kanda hiyo yanabidi yakome kuuza silaha zao nchini Sudan.
Mataifa ya kigeni katika vita vya Sudan
Japo mataifa hayo hayakutajwa moja kwa moja lakini inafahamika kwamba Jenerali Al Burhani ambaye aliliongoza jeshi kutwaa madaraka mwaka 2021 ni mshirika wa karibu wa nchi jirani na Sudan ya Misri na rais Abdel-Fatah Al Sisi ambaye aliwahi pia kuwa mkuu wa jeshi.
Lakini pia mwezi Februari waziri wa mambo ya nje wa Sudan alikwenda Tehran alikofanya mazungumzo na mwenzake zikiweko ripoti ambazo hazikuthibitishwa kwamba Sudan iliagiza Droni kutoka Iran.Kwa upande mwingine Hamdani Dagalo,kiongozi wa RSF anatajwa kupata msaada kutoka kundi la mamluki la Urusi Wagner lakini pia ripoti ya hivi karibuni ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilionesha RSF wanapokea pia msaada kutoka mataifa ya kiarabu.
Ikumbukwe kwamba miongo miwili iliyopita jimbo la Darfur lilitumbukia kwenye mauaji makubwa ya kimbari na ukashuhudiwa uhalifu mkubwa wa kivita na hasa hasa ule uliofanywa na wanamgambo wa jamii ya Wasudan wenye asili ya kiarabu wa kundi la Janjaweed dhidi ya Wasudan weusi. Zaidi ya watu 300,000 waliuwawa na milioni 2.7 walilazimika kuyakimbia makaazi yao na kuwa wakimbizi.